Miss Tanzania, Miriam Gerald, akiwa na ndugu zake kuelekea nyumbani baada kudhaminiwa na mkurugenzi wa mashindano hayo Hashim Lundenga kwenye mahakama ya hakimu mkazi Kinondoni jijini Dar es Salaam jana. Miriam pamoja na rafiki yake wa kiume Kenedy Victor wanashtakiwa kwa kosa la kujeruhi na kuharibu mali na wote wamekewa dhamana. Picha na Silvan Kiwal
******************************************************************************************************************
HATIMAYE Miss Tanzania 2009, Miriam Gerald ameachiwa kwa dhamana baada ya kukaa rumande kwa siku tatu, kuanzia Ijumaa mchana kwa kukosa dhamana.
Mrembo huyo wa mwaka jana, alipelekwa rumande kwa kile kilichoelezwa kushambulia pamoja na kuharibu mali.
Katika shtaka la kwanza, wanatuhumiwa kumshambulia Shaaban Moshi kwa vitu vyenye ncha kali shtaka lililosomwa na mwendesha mashtaka Inspekta wa Polisi, Nassor Sisiwahy, mbele ya Hakimu, Kwey Lusemwa.
Shitaka la pili, watuhumiwa kufanya uharibifu wa mali yenye thamani ya Sh laki 720,000. Mali iliyoelezwa ni vifaa vya muziki. Ijumaa walishindwa kutimiza masharti ya dhamana na kupelekwa Gereza la Segerea.
Hata hivyo, jana alipata dhamana pamoja na rafiki yake, Kennedy Victor.
Baada ya kuruhusiwa na mahakama, Mratibu wa Miss Tanzania, Hashim Lundenga aliwaomba radhi Watanzania kwa yanayotokea kwa washindi wa taji hilo.
Lundenga aliyasema hayo jana nje ya Mahakama ya Kinondoni baada ya kumwekea dhamana mrembo wake na kusema: "Hayo ni mambo ya kimaisha na yanaweza kumtokea yeyote."
Mrembo huyo aliwasili mahakamani hapo saa 5.15 asubuhi akiwa kwenye gari aina ya Land Cruizer STK 4253 ambalo liliingia Mahakamani hapo kwa kasi akiwa na wenzake wawili na Miriam alishuka akiwa amejifunika mtandio usoni.
Baada ya hapo, saa 11.30 washtakiwa hao walipandishwa kizimbani na Hakimu Richard Kabate ambaye aliwaachia kwa dhamana kwa niaba ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Kwey Lusema.
Wote walitimiza masharti ya dhamana yao na kuwataka kurudi tena mahakamani Februari 25 .
Lundenga alitoa dhamana hiyo kwa mrembo wake Miriam huku Kennedy akitolewa dhamana na rafiki yake Omary Juma Idd ambaye ni mfanyakazi wa Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana.
'' Siwezi kuongea mengi kwa kuwa kesi bado ipo mahakamani ila naweza kusema kuwa yaliyomtokea Miriam ni matatizo tu ya kimaisha hatutakiwi kumlaumu kwani mpaka sasa bado hatujajua kama kosa hilo katenda au la,'' alisema Lundenga.
Aidha Lundenga alisema kuwa kwa kitendo alichofanyiwa Miriam si cha kistaarabu na kamati yake inawatafuta warembo hao wanasheria na wanapopatwa na matatizo wawe wanaongea na sio warembo wenyewe. SOURCE: MWANANCHI
Comments