Richmond kwisha kazi!!!



BUNGE limefunga rasmi mjadala wa mkataba tata wa Kampuni ya Richmond Development (LLC) na Tanesco na kuacha serikali iendelee kutekeleza maazimio yake huku wabunge wawili Christopher Ole Sendeka na Dk Willibrod Slaa wakipambana hadi mwisho.

Dk Slaa na Sendeka wakionyesha ujasiri katika mapambano, sehemu kubwa ya wabunge wakiwemo wanaojipambanua kupambana na ufisadi jana walionekana kumezwa na kushindwa kung'ara huku Kamati ya Nishati na Madini yenye dhamana na sakata hilo, ikionyesha utiifu mkubwa kwa maamuzi ya serikali.

Tofauti na ilivyokuwa kwenye mkutano wa 16 wa Bunge na viapo vya baadhi ya wabunge kutaka kufa na Richmond, mjadala huo wa taarifa ya serikali kuhusu utekelezaji wa maazimio ya kampuni hiyo, ulianza kwa kupooza huku Mbunge wa Viti Maalumu (Ruvuma) Mhandisi Stella Manyanya, akiamua kuvirushia makombora vyombo vya habari na kusifia serikali na mawaziri wa serikali waliojiuzulu.

Lakini, Dk Slaa, ambaye alikuwa mchangiaji wa pili kwa mchana baada ya Juma Kilimbah, alianza kurusha makombora mazito akihoji ripoti kushindwa kubainisha mambo mengi ya msingi ambayo yalikuwemo kwenye taarifa kama hiyo iliyotolewa kwenye Mkutano wa 16 wa Bunge.

Kwa mujibu wa Dk Slaa, hakuelewa mantiki ya kukosekana majina ya watu muhimu waliopaswa kuwajibishwa kama aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini (Arthur Mwakapugi), kuachiwa hadi wanastaafu na wengine kutowajibishwa kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mbunge huyo wa Karatu na Katibu Mkuu wa Chadema, alihoji pia mantiki ya Kamati ya Nishati na Madini kumwacha Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Dk Edward Hoseah, kwa sababu nyepesi ya uchunguzi wa posho mbili unaofanywa na taasisi hiyo dhidi ya wabunge.

"Kuna mambo mengi ya msingi humu kwenye ripoti hayamo, kumwacha Hoseah kisa eti anafanya uchunguzi wa posho mbili dhidi ya wabunge ni jambo ambalo halina maana, kwa sababu hivi ni vitu viwili tofauti kabisa," alifafanua Dk Slaa.

"Kama ni uchunguzi wao kuhusu posho mbili waendelee na yeye kama ni kuwajibishwa hilo ni jambo jingine, kuliacha jambo hili katika mamlaka ya juu wakati Bunge ni chombo chenye nguvu na kushusha heshima ya Bunge."

Dk Slaa aliongeza kwamba, :"Uchunguzi wao waendelee kama mimi nimekula posho mbili wanichunguze waje wanikamate, lakini kuogopa uchunguzi wa Takukuru kuna walakini, nilikwishasema uchunguzi wa Takukuru usije ukafunga watu midomo."

Katika kuonyesha msisitizo, Dk Slaa aliweka bayana kwamba Dk Hoseah alionywa kwa kutokuwa makini na kutaka serikali ifafanue kama kosa hilo adhabu yake ya mwisho ni onyo au vinginevyo.

Mbunge huyo ambaye amejizolea sifa kutokana na kupambana na ufisadi, alihoji pia serikali kujaribu kusafisha hata wajumbe watano wa Timu ya Mashauriano ya Mikataba Serikalini (GNT), wakati walikuwa ni sehemu ya ushauri katika mkataba huo ambao uliitia serikali hasara.

Makombora hayo ingawa yalikuwa ya wabunge wawili, lakini yalitikisa Bunge, baada ya Sendeka kupata nafasi na kuhoji kama dhima za Bunge la kidemokrasia linavyoweza kufanya katika kusimamia rasilimali za taifa zisiporwe na watu mbalimbali wakiwemo wageni kwa kisingizio cha uwekezaji.

"Tumejiuliza kama mabunge ya wenzetu ya kidemokrasia yanafanya nini katika kusimamia rasilimali za taifa, sauti ya wanyonge na kupigania haki bila hofu na kufanya mambo kwa ujasiri?"
imeandikwa na Ramadhan Semtawa na Exuper Kachenje, Dodoma.

Comments