Friday, October 19, 2007

Papa Benedict 16 kuja bongo



KIONGOZI wa Kanisa Katoliki duniani Baba Mtakatifu, Papa Benedict 16, amekubali mwaliko wa Rais Jakaya Kikwete kuitembelea Tanzania katika ziara yake anayotarajia kuifanya hivi karibuni katika nchi za bara la Afrika.

Rais Kikwete alitoa mwaliko huo jana wakati wa mazungumzo yake na Baba Mtakatifu yaliyofanyika katika maktaba yake iliyoko katika Makao Makuu ya Kanisa Katoliki, Vatican, Italia.

Akizungumza katika mkutano huo Papa Benedict 16 alisema ataitembelea Tanzania katika ziara yake hiyo ili kuendeleza uhusiano uliopo baina ya nchi hizo mbili ulioanza tangu enzi za uhai wa baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.

"Tanzania tunaipa umuhimu wa pekee, ni nchi ambayo haina matatizo ya watu kugombana kwa sababu ya tofauti ya dini au rangi zao, ninafurahishwa sana na hali ya watu kuishi kwa pamoja na kwa amani na ninakupongeza kwa kuendeleza hali hii, hili ni jambo linalonifurahisha. Nitaendelea kuiombea Tanzania ili iendelee kuwa nchi ya amani," alisema Baba Mtakatifu huyo.

Mbali na kukubali wito huo Baba Mtakatifu alimwahidi rais Kikwete kuwa Kanisa Katoliki Duniani litaendelea kuisadia Tanzania kwa kuchangia huduma muhimu za maendeleo bila kujali tofauti za dini baina ya wananchi.

Alisema Tanzania ni nchi ambayo inahitaji msaada hasa katika upatikanaji wa elimu kwa wananchi ili kuwawezesha kukabiliana na janga la ukimwi kwa ufanisi.

Rais Kikwete alipata fursa ya kuzungumza na Baba Mtakatifu huyo kwa mwaliko wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio kuwa mgeni rasmi katika mkutano wa kimataifa wa madhehebu mbalimbnali ya dini duniani katika mkutano uliofanyika Napoli.

Akazungumza katika mkutano huo Baba Mtakatifu alimpongeza Rais Kikwete kwa kuendeleza amani na utulivu nchini Tanzania

Aliisifia Tanzania kwa kuendelea kuwa kama ilivyo kwa kuwa viongozi wake wameendelea na kuienzi misingi mizuri ya uongozi ambayo iliasisiswa na hayati Mwalimu Nyerere.

No comments: