NI kama vile taarifa ya kufurahisha, lakini iliyojaa mzaha mwingi na yenye lengo bila shaka la kufuta hasira za walalala hoi wa mitaani wanaotaabika kwa udi na uvumba wakisaka mkate wao wa kila siku. Serikali imetangaza rasmi kima cha chini cha mshahara katika sekta binafsi huku wafanyakazi wa majumbani wakipangiwa Sh 65,000, wafanyakazi wa sekta ya madini Sh 350,000 na wahudumu wa baa na nyumba za kulala wageni Sh 80,000 kwa mwezi na kitaanza kutumika rasmi Novemba Mosi.
Viwango hivyo vipya vimetokana na utafiti uliofanywa na Bodi ya Uchunguzi wa Mishahara katika sekta binafsi, ambayo iliteuliwa Aprili mwaka huu na Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, John Chiligati, kufuatia Sheria mpya ya Kazi namba 7/2004, kifungu namba 35 (1).
Akitangaza mishahara hiyo jijini Dar es Salaam jana, Waziri Chiligati, alisema viwango hivyo vipya vya kima cha chini vitahusu wafanyakazi wa sekta binafsi pekee.
Alisema mishahara hiyo mipya inagusa sekta zote ikiwemo ya kilimo, madini, afya, biashara na viwanda, ulinzi wa makapuni binafsi, huduma za usafiri na mawasiliano, maji, pamoja na wafanyakazi wa majumbani na mahotelini. Bonyeza hapa upate kusoma habari hii ya gazeti la Mwananchi kwa kina zaidi.
Comments