Saturday, October 20, 2007

Ndesamburo amtaka kikwete kuvunja baraza la mawaziri

Na Ally Sonda, Moshi wa Mwananchi

MBUNGE wa Moshi Mjini (CHADEMA) , Phillemon Ndesamburo amemuomba Rais Jakaya Kikwete kuvunja Baraza la Mawaziri na kuendesha nchi kwa kuwatumia Makatibu wakuu wa wizara,ili kutoa nafasi ya kuunda serikali yake upya.

Mbunge huyo alitoa ombi hilo jana wakati akihojiwa na Mwananchi,nyumbani kwake mtaa wa Mbokomu mjini hapa Mkoa wa Kilimanjaro wakati akizungumzia tuhuma za ufisadi dhidi ya viongozi wa serikali.

Ndesamburo aliwashambulia Jaji Joseph Warioba na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Siasa), Kingunge Ngombale Mwiru kwa madai kuwa kauli zao zinatetea ufisadi nchini.

mbunge huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Kilimanjaro, aliwataka Warioba na Kingunge kuondoa laana katika makaburi yao pindi watakapokufa kutokana na kutetea udhalimu uliofanywa na baadhi ya vigogo wa serikali kwa kuitia hasara nchi wakati wananchi wengi ni maskini.

Akizungumzia uimara wa Serikali ya Kikwete, Ndesamburo, alisema imepwaya kutokana na viongozi wake muhimu kutuhumiwa kwa rushwa na kushindwa kuwachukulia hatua za kinidhamu dhidi yao.

Alionya kama Kikwete hatavunja Baraza la Mawaziri waliotajwa kwenye kashfa ya ufisadi na a na kufanya kazi na makatibu wakuu, nchi inaweza kuingia kwenye vurugu.

Vilevile alitakawote waliotajwa kuhusika na rushwa za mikataba ya madini na zile za ulaji wa mabilioni ya fedha za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kuchunguzwa na taasisi binafsi, zikiwemo za kimataifa.

Kwa upande mwingine, alisema kitendo cha Kikwete kuacha kuzunguzia suala la ufisadi na kuamua kusafiri nje ya nchi ni kielelezo tosha kuwa, anaogopa kuwachukulia hatua za kinidhamu waliotajwa kuhusiana nao.

Alisema Kikwete anapaswa kuheshimu kauli na mawazo yaliyotolewa na viongozi waandamizi waliowahi kuingoza Tanzania kama vile Alli Hassan Mwinyi, Dk Salim Ahmed Salim, Jaji Paul Bomani na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, John Malecela.

Alisema Watanzania wakiwamo viongozi wa vyama vya upinzani wanamuombea kila la kheri na afya njema Kikwete ili aweze kuongoza nchi kwa amani na utulivu hadi mwaka 2010.

No comments: