Monday, October 15, 2007

Mwamunyange awavisha vyeo makamanda JWTZ

Na Kizitto Noya

MKUU wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange, amewavisha vyeo vipya maafisa wakuu 19 wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliopandishwa vyeo mwishoni mwa wiki iliyopita na Rais Jakaya Kikwete.

Jenerali Mwamunyange aliwavisha vyeo hivyo jana na kuwapangia nyadhifa mpya maafisa wanane kati yao katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Waliopangiwa nyadhifa mpya ni Meja Jenerali Wyanjones Kisamba, aliyekuwa Kamanda wa Brigedi ya Kaskazini Arusha, ambaye sasa anakuwa mkuu wa kwanza wa Kamandi mpya ya Majeshi ya Nchi Kavu ambayo imeundwa kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa JWTZ mwaka 1964.

Kabla ya kuundwa kwa kamandi hiyo ,JWTZ ilikuwa na komandi mbili ambazo ni Navy, kwa ajili ya vikosi vya maji, Kamandi ya Ulinzi wa Anga kwa ajili ya vikosi vya Anga na brigedi za vikosi vya nchi Kavu.

Kamandi mpya iliyoundwa itaunganisha brigedi zote za askari wa miguu pamoja na vikosi vya vifaru, mizinga na uhandisi wa medani.

Maafisa wengine waliopangiwa nyadhifa mpya ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Wanawake Jeshini, Meja Jenerali Zawadi Madawili ambaye sasa ni Mkuu wa tawi la Mgambo, Brigedia Jenerali Vicent Mritaba anayekuwa Kamanda wa Brigedi ya Magharibi Tabora na Brigedia Jenerali Charles Kitenga aliyeteuliwa kuwa Kamanda wa Brigedi ya Kaskazini badala ya Meja Jenerali Kisamba.

Wengine ni Brigedia Jenerali Patrick Mlowezi aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Shule ya Huduma Pangawe, Brigedia Jenerali Charles Mzanila anayekuwa Meneja Mkuu wa kiwanda cha mazao Morogoro, Brigedia Jenerali Lilian Kingazi kuwa Mkurugenzi wa Utumishi jeshini na Brigedia Jenerali Grace Mwakipunda kuwa Mkurugenzi wa Musuala ya wanawake jeshini.

Maafisa wakuu waliobaki ambao wanaendelea na nyadhifa zao za awali ni Msemaji wa Wizara ya Ulinzi na JKT, Meja Jenerali Alfred Mbowe, Kamanda wa Brigedi ya Mashariki, Dar es Salaam, Meja Jenerali Servas Hinda na Mabrigedia Jenerali Kelvin Msemwa, Albert Kigadye, Sebastian Chiwangu, DAniel Igoti, Salum Kijuu, Farrah Mohamed, Gerald Kiswaga, Julius Mbilinyi na Mabula Mashauri.

No comments: