Serikali yawapigia magoti wafadhili



HATIMAYE serikali imekubali kuchunguza tuhuma za ufisadi wa mabilioni ya fedha za umma zilizotolewa na Mbunge wa Karatu (Chadema), Dk Willibrod Slaa, dhidi ya vigogo 11 na kuonya kuwachukulia hatua za kisheria au kuwawajibisha watakaopatikana na hatia.

Hatua hiyo imechukuliwa ikiwa ni siku chache baada ya mabalozi wa nchi mbalimbali, ikiwamo Uholanzi Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU), Marekani, Ujerumani, Benki ya Dunia na viongozi wa dini kuitaka serikali kutoka tamko linaloeleweka na la wazi kuhusu tuhuma hizo.

Uamuzi huo ulitangazwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe kwa niaba ya serikali, alipozungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari, jijini Dar es Salaam jana na kauli hiyo pia aliirudia jana mchana alipokutana na mabalozi wa nchi za nje wanaowakilisha nchi zao Tanzania.

Waziri Membe alisema ana uhakika Rais Jakaya Kikwete na serikali yake ya awamu ya nne, atahakikisha baada ya uchunguzi wa tuhuma hizo kukamilika, wahusika wanachukuliwa hatua za kisheria au kuwajibishwa.

Comments