Tuesday, October 02, 2007

Makatibu wakuu 15 kutembelea Buzwagi

Bw. Gray Mgonja Katibu Mkuu Hazina, sijui kama na yeye atakuwamo.

*Hazina ya dhahabu Tulawaka ukingoni

Na Mwandishi Wetu wa Mwananchi

MAKATIBU wakuu kutoka wizara 15 wanatarajiwa kuanza ziara ya kutembelea migodi ya dhahabu Buzwagi, North Mara, Bulyanhulu na Tulawaka ambayo inamilikiwa na Barrick ili kuona shughuli zinazofanywa na kampuni hiyo.

Akizungumza na Mwananchi, Afisa Mwandamizi wa Mawasiliano wa Barrick Tanzania, Teweli Teweli alisema lengo la ziara hiyo ni kuelimisha wadau mbalimbali kuhusiana na sekta ya madini.

"Ziara hiyo ni mpango wa Barrick ambao una lengo la kuelimisha wadau mbalimbali wakiwamo waandishi wa habari, viongozi wa serikali kuhusiana na sekta ya madini, watu wengi bado hawajui mambo mengi ya sekta hii mpya Tanzania," alisema.

Tayari Kampuni ya Barrick imeshapeleka baadhi ya wahariri wa habari kutembea mgodi wa Bulyanhulu na Tulawaka mwishoni mwa wiki iliyopita kwa dhumuni hilo. Wahariri hao ni kutoka magazeti ya Mtanzania, This Day, Mwananchi na kutoka Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).

Ratiba ya safari hiyo inaonyesha kwamba makatibu wakuu hao wataondoka jijini Dar es Salaam Jumamosi alfajiri na kuwasili Bulyanhulu saa tatu asubuhi na kupata maelezo mafupi kisha kwenda kwenye ndani ya mgodi kuangalia shughuli za uchimbaji madini zinavyoendelea. Siku hiyo pia watatembelea shughuli za maendeleo ambazo mgodi huo unafanya kwa wanakijiji wanaozunguka maeneo hayo.

Siku ya pili, ratiba inaonyesha kwamba makatibu hao wakuu watakwenda katika mgodi wa Tulawaka ulioko mkoani Kagera katika wilaya ya Biharamulo kwa ajili ya kutembea sehemu za machimbo na kuangalia programu ya utunzaji mazingira katika eneo hilo. Siku hiyo wataenda katika mgodi wa North Mara na Buzwagi kwa ajili ya shughuli za kukagua mgodi.

Wakati huo huo, mgodi wa Tulawaka ambao ulianza uzalishaji 2005 unatarajia kumaliza hazina yake ya madini ya dhahabu 2010 ikiwa ni miaka miwili imebakia sasa.

Meneja Mkuu wa Mgodi wa Talawaka, Scott Artkinson aliwaambia waandishi wa habari waliotembelea mgodi huo mwishoni mwa wiki iliyopita kwamba hazina ya madini katika mgodi huo inatarajia kuisha miaka miwili ijayo na hivyo kama hawatagundua hazina zaidi, mgodi huo utafungwa.

"Mgodi utakamilisha shughuli zake 2010, lakini tunaweza kugundua hazina ya madini wakati tukiendelea na uchimbaji," alisema.

Tofauti na migodi mingine inayomilikiwa na Barrick, Mgodi wa Tulawaka unatoa dhahabu tu na kiwango chake cha ubora ni kikubwa. "Kuanzia mwaka jana, tumeanza kupata faida, kwa hiyo mgodi wetu unajiendesha kwa faida," alisema

Artkinson alisema kwamba mwaka jana mgodi ulipata faida ya Sh9 bilioni na mwaka huu wanatarajia kupata faida ya Sh13bilioni.

No comments: