Wednesday, April 01, 2015

SHIRIKA LA TAIFA LA BIASHARA ZANZIBAR (ZSTC) LIMETOA VIFAA KWA WAKULIMA WA KARAFUU MKOA WA KASKAZINI UNGUJA

01
Mkurugenzi Mipango na Utawala wa Shirika la ZSTC Ussi Muhamed Juma (aliyesisimama) akizungumza na wanavikundi vya kuatika miche ya mikarafuu kabla ya kukabidhi vifaa vya kuatikia miche hiyo vyenye thamani ya zaidi ya Sh/Milioni 5 katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kaskazini  Unguja, kulia Katibu Tawala Mkoa huo Omar Hassan Masoud.
02
Baadhi ya wanavikundi vya kuatika miche ya mikarafuu wakimsikiliza Mkurugenzi Mipango na Utawala wa ZSTC  (hayupo pichani) katika hafla ya kuwakabidhi vifaa kwa ajili ya kukendeleza shughuli zao.
03
Katibu Tawala wa Mkoa Kaskazini Unguja Omar Hassan Masoud akimkabidhi Mwanaharusi Haji Muhammed wa kikundi cha Mungu tupeheri cha Donge mnyimbi vifaa hivyo kwa ajili ya kuendeleza kazi zao za kuatika miche ya mikarafuu.
04
Miongoni mwa  vifaa vilivyotolewa na Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar  (ZSTC) kwa wanavikundi vya kuatika miche ya mikarafuu.
05
Mmoja ya wanavikundi vya kuatika miche ya mikarafuu Saidi Khatib Juma akitoa shukrani ZSTC kwa kuwapatia vifaa vya kuendeleza kazi zao.
06
Picha ya pamoja ya wanavikundi vya kuatika miche ya mikarafuu pamoja na wafanyakazi wa Shirika la ZSTC.
…………………………………………………………………….
Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar.
Vifaa mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya Shl Million 5 unusu vimegawiwa kwa Vikundi nane vinavyojishughulisha na Uatikaji wa Miche ya Mikarafuu Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Ugawaji huo wa Vifaa ni mwendelezo wa Juhudi za makusudi zinazofanywa na Shirika la Biashara la Taifa ZSTC ili kuwasaidia Wakulima wa zao la Karafuu katika kuliinua zao hill.
Akigawa Vifaa hivyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Katibu Tawala wa Mkoa huo Omar Hassan Masoud Masoud amesema vitawasaidia sana Wakulima hao katika kuliendeleza zao hilo la Kibiashara.
Amesema mafanikio ya ZSTC katika zao la Karafuu kuanzia kwa Wakulima hadi katika Soko la Dunia yanatokana na juhudi za makusudi zilizopangwa na Serikali kuliimarisha zao hilo.
Katibu huyo amesema juhudi hizo zimeongeza kiwango cha uzalishaji, usafirishaji na Ubora wa zao hilo kutokana na kuongezwa kwa bei ambapo Mkulima hupata Asilimia 80 ya Bei ya Soko la Dunia.
Katibu Omar ameongeza kuwa bei hiyo imewawezesha Wakulima kumudu gharama za uzalishaji kama vile kuotesha miche hadi Karafuu kuzaliwa.
Itakumbukwa kuwa Karafuu ndio zao pekee linalochangia kwa kiasi kikubwa Pato la Taifa
kuliko zao jingine ambapo katika kipindi cha Mageuzi ya Sekta ya Karafuu huchangia kwa Wastani wa Asilimia 20.49.
Kwa upande wao Wakulima waliopewa Vifaa hivyo vya kuatikia Miche wamelishukuru Shirika la ZSTC kwa kuendelea kuwa Karibu nao na kusikiliza mahitaji yao.
Mmoja wa Wakulima hao Mwanakhamis Haji Mohamed msaada huo umekuja wakati muafaka na kwamba utawaongezea Ari ya kuliendeleza zao hilo.
Awali akitoa nasaha zake Mkurugenzi Mipango na Utawala wa ZSTC Ussi Mohamed Juma amesema Serikali imeanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Karafuu ili kuwezesha ufanisi katika kuliinua zao hill.
Amesema Mfuko huo ndio unaohusika katika kutoa Misaada, Mikopo na Pembejeo na kuwataka Wananchi kuanzisha Vikundi vyao ili kupata wepesi wa kusaidiwa.

Baadhi ya Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na Matenki ya kuhifadhia maji, Mapauro, Mabero, Keni, Pampu za Maji na Vifuko vya Kuatikia Miche ya Mikarafuu.

Vikundi vilivyopata Msaada huo leo ni pamoja na Mungu tupe Kheri, Tumaini, Tupendane, Mshirika wa Mikarafuu na Mikarafuu Cooperate Society.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea kufanya juhudi mbali mbali za kulifanya zao hilo kuwa Sekta Kiongozi ya Uchumi ambapo kila Mwaka hugawa Miche Million moja kwa Wakulima Unguja na Pemba.

No comments: