Friday, February 27, 2015

SERIKALI KUFUFUA BANDARI 14 ZA ZIWA NYASA – WAZIRI MKUU


*Apewa jina la Chifu wa Wanyakyusa, aitwa Mwakabulufu 
WAZIRI MKUU Mizengo amesema Serikali imeamua kufufua bandari ndogo 14
kwenye mikoa mitatu inayozunguka Ziwa Nyasa ili kuimarisha usafiri wa
majini kwa wakazi wa Ruvuma, Njombe na Mbeya.
 
“Tangu mwaka 2006 bandari za kwenye mikoa ya Ruvuma, Njombe na Mbeya
zilikufa na hivyo kuleta shida ya usafiri kwa wakazi wa maeneo hayo
lakini Serikali imeamua kuzifufua bandari hizo na Itungi itakuwa ndiyo
kituo kikuu cha bandari zote katika Ziwa Nyasa,” alisema Waziri Mkuu.
 
Alikuwa akizungumza na wakazi wa Wilaya ya Kyela kwenye mkutano wa
hadhara uliofanyika jana jioni (Jumatano, Februari 26, 2015) kwenye
uwanja wa michezo wa Mwakangale na kuhudhuriwa na maelfu ya wakazi wa
wilaya hiyo.
 
Alizitaja bandari hizo kuwa ni Ndumbi, Lundu, Njambe, Mkili, Liuli, na
Mbamba bay ambazo ziko mkoani Ruvuma. Nyingine ni Lumbila, Ifungu,
Nsisi, Lupingu na Manda ambazo ziko Njombe wakati bandari za Mbeya ni
Itungi, Kiwira na Matema.
 
Alisema ili kufanikisha hilo, Serikali imehamisha chelezo (Dry Dock)
kutoka bandari ya Mwanza na kwamba mkandarasi kutoka Kampuni ya
Songoro Marines, ameshaanza  ujenzi wa chelezo hiyo.
 
“Baada ya kukamilika, Chelezo hiyo, itatumika kutengenezea meli mpya
yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 200 za mizigo na kufanya
ukarabati wa meli pindi zinapohitaji matengenezo. Nimeambiwa na
mkandarasi kutaka watamaliza hii kazi ifikapo Juni, mwaka huu,”
alisema huku akishangiliwa na umati huo.

No comments: