Friday, February 27, 2015

JAJI KIONGOZI ATOA SOMO KWA WATUMISHI WA MAHAKAMA, VYAMA VYA WAAJIRI NA WAAJIRIWA.

JA1
Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Shaaban Lila akifungua mkutano maalum wa watendaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Chama cha waajiri Tanzania (ATE) na Wafanyakazi (TUCTA) leo jijini Dar es salaam. Mkutano huo unalenga kuangalia na kutafuta majibu ya changamoto mbalimbali zinazohusu maslahi ya wafanyakazi na mashauri yanayopelekwa mahakama Kuu Divisheni ya Kazi nchini.
JA2
Baadhi ya washiriki wa mkutano maalum wa watendaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Chama cha waajiri Tanzania (ATE) na Wafanyakazi (TUCTA) wakifuatilia masuala mbalimbali leo jijini Dar es salaam.
JA3
Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Shaaban Lila akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua mkutano maalum wa watendaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Chama cha waajiri Tanzania (ATE) na Wafanyakazi (TUCTA) leo jijini Dar es salaam.
……………………………………………………………………………….
Na. Aron Msigwa – MAELEZO
Dar es salaam.
Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Shaaban Lila ametoa wito kwa watendaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi nchini  kufanya kazi kwa kuzingatia weledi, viwango na uadilifu ili mahakama hiyo iendelee kuwa kimbilio la wananchi wanaotafuta haki.
Akizungmza wakati wa wakati wa kikao cha wadau wa Mahakama kujadili uboreshaji wa utendaji kazi katika Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi kilichowahusisha watendaji wa Mahakama ya Kazi , Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) leo jijini Dar es slaam, Mhe.Shaaban Lila amesema kuwa  msingi mkuu wa Mahakama ya Tanzania nikuhakikisha kuwa inatoa maamuzi kwa wananchi kwa haki na wakati.
Amesema  iwapo waajiri na waajiriwa kote nchini haki watazingatia wajibu wao katika kutekeleza majukumu yao kulingana na kanuni na taratibu zinazosimamia maeneo ya kazi migogoro  mingi inayopelekwa mahakamani baina ya waajiri na waajiriwa itapungua nchini.
 “Kila upande ifanye kazi yake kwa haki ,kumekuwa na mrundikano wa mashauri  ya kazi yanayokwenda mahakamani kwa ajiri ya utatuzi na usuluhishi ,mengi ya mashauri hayo hayahusiani na kufukuzwa kazi isipokuwa yale ya kukosa uaminifu, wizi na ubadhirifu sehemu za kazi” Amesisitiza.
Amebainisha kuwa Mahakama ya Tanzania lazima iheshimiwe kutokana na misingi yake kwa kuweka msisitizo katika kushughulikia masuala ya msingi na kutatua kero za wananchi hususan usimamizi na utoaji wa haki kwa wakati.
Mhe. Shaaban amefafanua kuwa Mahakama ya Tanzania inaendelea kufanya maboresho na mabadiliko katika kushughulikia mashauri ya muda mrefu yaliyoko mahakamani huku akieleza kuwa mkakati wa sasa ni kupunguza umri wa mashauri ya muda mrefu ya miaka 5 hadi 10 yanayofikia 265  na yale ya umri wa miaka 3 yapatayo 201 yaweze kushughulikiwa ndani ya mwaka 1 hadi 2 ifikapo June 2015.
“Lengo letu ni kushughulikia mashauri haya haraka kwa muda mfupi, muhakikishe mashauri haya mnayamaliza kwa sababu yanagusa uzalishaji na maisha ya watu, kuchelewa  kuyasikiliza  kunaathiri  uchumi ” Amesisitiza.
Aidha,amewataka wadau wanaoshiriki mkutano huo kujipima katika malengo wanayojiwekea pamoja na kusimamia utekelezaji wa hukumu na maamuzi yanayotolewa na mahakama na kueleza kuwa ofisi yake inaandaa mkakati wa usimamizi wa suala hilo.
 Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Waajiri nchini Tanzania (ATE) Dkt. Aggrey Mulimuka akizungumza katika mahojiano maalum amesema kuwa mbali na mkutano huo kuwaweka pamoja wadau  hao kwa maana ya Mahakama, Waajiri (Serikali) na waajiriwa unalenga kuangalia na kutafuta majibu ya changamoto mbalimbali zinazohusu maslahi ya wafanyakazi na mashauri yanayopelekwa mahakama Kuu Divisheni ya Kazi nchini.
Amesema asilimia 70 ya mashauri yanayokwenda  mahakama Kuu Divisheni ya Kazi yanahusu migogoro ya waajiri  kuwasimamisha kazi wafanyakazi wao kutokana na makosa mbalimbali na kuongeza  kuwa mengi ya makosa hayo hayasababishi mtu afukuzwe kazi.
Ametoa wito kwa pande zote kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia maadili, kufuata haki ili mashauri yote yanayopelekwa mahakamani yaweze kupatiwa ufumbuzi wa kudumu na kuondoa migogoro ya kazi inayojitokeza katika maeneo mbalimbali nchini.

No comments: