NAIBU WAZIRI WA MAJI, AMOS MAKALLA ATEMBELEA WILAYA YA LONGIDO, MKOANI ARUSHA

1
Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla na Mkuu wa Wilaya ya Longido, James Ole Millya wakipanda mlima kuelekea kwenye eneo la mradi wa maji wa Kijiji cha Gelai-Meirugoi, Wilaya ya Longido, Mkoani Arusha.
2
Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla akiweka jiwe la msingi la mradi wa maji wa Kijiji cha Gelai-Meirugoi, Wilaya ya Longido, Mkoani Arusha.
3
Mradi wa maji wa Kijiji cha Gelai-Meirugoi.
4
Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla akiwa katika picha ya pamoja na akina mama wa Kijiji cha Gelai-Meirugoi, Wilaya ya Longido, Mkoani Arusha.
……………………………………………….
Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla jana ametembelea Wilaya ya Longido, Mkoani Arusha kwa mara ya kwanza kama Naibu Waziri wa Maji na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa maji wa Kijiji cha Gelai-Meirogui.
“Leo nina furaha ya kufika Longido kwa mara ya kwanza kama Naibu Waziri wa Maji, lakini pia kama kiongozi . Nia yangu ni kuja kuleta ufumbuzi wa tatizo la maji la muda mrefu Longido, kwani ni wilaya yenye kero kubwa ya maji katika mkoa wa Arusha. Wizara ya Maji imechukua hatua ya dharura kutatua tatizo hili”, alisema Mhe. Makalla. 
Naibu Waziri alisema kuwa utafiti wa visima vitano umefanyika na maeneo yatayochimbwa visima hivyo yamebainishwa tayari kwa kuchimba visima katika vijiji vitano, na zoezi hilo litaanza mara moja na litatekelezwa na Wakala wa Uchimbaji Visima na Mabwawa (DDCA) mpaka maji yapatikane katika visima hivyo vitakavyochimbwa.
Hatua hii inatokana na mkandarasi aliyekua akitekeleza mradi huo, kushindwa na kusababisha mradi huo kutokamilika. Hivyo, Wizara ya Maji kuamua kuchukua hatua kuhakikisha mradi unakamalika haraka iwezekanavyo na Sh. Mil 178 zimeidhinishwa kufanikisha zoezi hilo.
“Wizara ya Maji na TAMISEMI tutashirikiana kupitia ripoti ya utekelezaji wa mradi wa Longido na tutachukua hatua kali, za kinidhamu na kisheria kwa ngazi zote husika kuanzia mkandarasi na wataalamu wote waliochangia kutokukamilika kwa mradi huu wa Longido”, alisema Mhe. Makalla.
Ziara ya Naibu Waziri wa Maji wilaya ya Longido, imebainisha uongo wa taarifa iliyoripotiwa na gazeti moja siku za nyuma, iliyosema kwamba Mhe. Makalla alifanya uzinduzi wa mradi huo feki utoao matope baada ya maji, kitu ambacho si ukweli kwa kuwa hakuwahi kutembelea wilaya hiyo kabla ya jana.

Comments