Wednesday, October 29, 2014

Wananchi waaswa kuwa makini na kauli za wanasiasa-IPTL

 Katibu na Mshauri Mkuu wa Makapuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na Pan African Power Solutions (T) Limited (PAP), Bw. Joseph Makandege, (mwenye suti nyeusi kushoto) akimkabidhi Mwinjilisti wa Kanisa la KKKT Usharika wa Likamba Wilayani Arumeru, mkoani Arusha, Bi Martha Musa Kivuyo (mwenye nguo nyeupe), mfano wa hundi ya Shilingi milioni 10 kati ya Silingi milioni 20 (Tsh 20m/-) iliyotolewa na kampuni ya IPTL/PAP, kusaidia kwaya ya Patano la Usharika wa Likamba kuweza kurekodi albam ya nyimbo za injili.  

 Katibu na Mshauri Mkuu wa Makapuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na Pan African Power Solutions (T) Limited (PAP), Bw. Joseph Makandege, (mwenye suti nyeusi kushoto) akipongezwa na Mdhamini na Mlezi wa kwaya ya Patano la Usharika wa Likamba kanisa la KKKT la Arumeru, mkoani Arusha, Bw. Philip Makini baada ya kukabidhi  mfano wa hundi ya Shilingi milioni 10 kati ya Silingi milioni 20 (Tsh 20m/-) iliyotolewa na kampuni ya IPTL/PAP, kusaidia kwaya ya Patano la Usharika wa Likamba kuweza kurekodi albam ya nyimbo za injili. Wakishuhudia ni Mwinjilisti wa Kanisa hilo, Bi Martha Musa Kivuyo (mwenye nguo nyeupe), na Meneja Uhusiano wa Jamii wa IPTL/PAP Bw. Sylvester Joseph pamoja na wanakwaya. 
 Katibu na Mshauri Mkuu wa Makapuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na Pan African Power Solutions (T) Limited (PAP), Bw. Joseph Makandege, (kulia) akizindua albam mpya ya nyimbo za injili ya kwaya ya Patano la Usharika wa Likamba Kanaisa la KKKT la Wilaya ya Arumeru, Arusha. Kati kati ni Meneja Uhusiano wa Jamii wa Makampuni ya IPTL/PAP Bw. Sylvester Joseph akifuatwa na Bi.Hellen Zelothe.
 Katibu na Mshauri Mkuu wa Makapuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na Pan African Power Solutions (T) Limited (PAP), Bw. Joseph Makandege, (kulia) akionyesha albam mpya ya nyimbo za injili ya kwaya ya Patano la Usharika wa Likamba Kanaisa la KKKT la Wilaya ya Arumeru, Arusha mara tu baada ya kuuzindua. Wakishuhudia kutoka kulia ni Mfadhili na mlezi wa kwaya hiyo Bw. Philip Makini, ambaye pia ni Afisa Mwandamizi wa jumuia ya Afrika Mashariki, akifuatwa na Meneja Uhusiano wa Jamii wa Makampuni ya IPTL/PAP Bw. Sylvester Joseph akifuatwa na Bi.Hellen Zelothe.
 Moja wa waumini katika Kanisa la KKKT Usharika wa Likamba iliyopo Wilaya ya Arumeru mkoa wa Arusha, Bw. Thedayo Zelothe (kulia) akitoa mchango wake wa fedha pamoja na jogoo wawili wakato wa harambee ya kuchangia kwaya ya Patano la kanisa hilo mwishoni mwa wiki kwa lengo la kurekodi albam ya nyimbo za injili. Aliyebeba majogoo ni Mgeni rasmi katika harambee hiyo ambaye ni Katibu na Mshauri Mkuu wa Makapuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na Pan African Power Solutions (T) Limited (PAP), Bw. Joseph Makandege. Wakishuhudia ni Mfadhili na mlezi wa kwaya hiyo Bw. Philip Makini (wa pili kulia), Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CCK) Bw. Renatus Mwabih (wa pili kushoto) akifuatwa Bi.Hellen Zelothe. 

 Katibu na Mshauri Mkuu wa Makapuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na Pan African Power Solutions (T) Limited (PAP), Bw. Joseph Makandege, (wa pili kulia) akimpongeza mototo aliyeonyesha umahiri wake wa kucheza na kuimba nyimbo za injili akiwa ni mwanakwaya ya Edeni ya Kanisa la Morovian la Mjini Arusha. Mgeni rasmi alitoa Shilingi milioni moja (Tsh 1m/-) kama mchango wa ada yake ya shule. 

Wananchi wametakiwa kuwa makini na kauli za wanasiasa kwani sio kila kitu wanachosema ni cha kweli bali baadhi yao hupotosha jamii kwa maslahi yao binafsi.

Akizungumza wakati wa harambee ya kuchangia kwaya ya Patano la Kanisa la KKKT Usharika wa Likamba Wilayani Arumeru-Magharibi, Mkoani Arusha mwishoni mwa wiki, Wakili ambaye pia ni Katibu na Mshauri Mkuu wa Sheria wa makapuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na Pan African Power Solutions (T) Limited (PAP), Bw. Joseph Makandege, (ambaye alimwakilisha Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPTL/PAP, Bw. Harbinder Singh Sethi) alionya kuwa kauli za upotoshaji katika maswala mbali mbali nchini, hususan ya kisheria zinaweza kuleta madhara makubwa sana kwa taifa.

“Kama mwanasheria, ningependa kuwashauri wanasiasa wetu kuacha kuingilia mashauri yaliyopo mahakamani au ambayo yameamuliwa na vyombo halali vya kimahakama kwa kutoa kauli ambazo  zinawapotosha wananchi. Wakiendelea na tabia ya kuhoji uhalali wa maamuzi ya mahakama, itapelekea hata wananchi kutokuwa na imani na mahakama zetu, jambo ambalo linaweza kusababisha haki za watu wanyonge kupotea na amani ya nchi yetu kutoweka,” alisema Bw. Makandege.

Aliongeza kuwa kauli hizo zinachangia kuiathiri jamii ambayo pengine hawajui ukweli kuhusu jambo linaloongelewa kwa kuwa wengi wao wanaamini kuwa kila kauli ya mwanasiasa ina ukweli na inapotokea mwanasiasa anaipotosha jamii madhara yake huwa makubwa sana. 

Mwanasheria huyo akitolea mfano tuhuma zinazo endelea kuhusu kutwaliwa kwa kampuni ya IPTL na PAP pamoja na fedha za IPTL zilizokuwa katika Akaunti ya Escrow ya Tegeta (IPTL Tegeta Escrow Account) katika Benki Kuu ya Tanzania, alisema licha ya wanasiasa  kutambua ukweli kwamba akaunti hiyo na fedha zote zilizokuwemo hazikuwa za umma, bado wanaendelea kuiongopea jamii kwamba fedha hizo zilikuwa mali ya umma, bila hata kuhofia madhara yanayoweza kusababishwa na kauli zao, jambo ambalo alisema kuwa linakinzana hata na maandiko matakatifu. 

Aliongeza kuwa kauli kama hizo sio tu zinahatarisha amani ya taifa letu kwani ni za kichochezi kwa sababu zinaweza kuwafarakanisha wananchi na serikali yao, bali pia zinaweza kuathiri uwekezaji katika nchi yetu kwa kuwakatisha tamaa wawekezaji jambo ambalo linaweza kuhatarisha uchumi wa taifa letu.

Akifafanua, Bw. Makandege alisema ukweli ni kwamba fedha zote zilizokuwa katika akaunti hiyo ya Escrow hazikuwa za umma bali zilikuwa fedha halali za IPTL, ambazo zilihifadhiwa katika akaunti hiyo ya Escrow kufuatia mgogoro baina ya wabia wa IPTL, Mechmar Corporation (Malaysia) Berhad (“Mechmar”) na VIP Engineering & Marketing Limited (“VIP”). Baada ya mgogoro kuisha kufuatia uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania (Mh. Jaji Utamwa) tarehe 5 Septemba 2013, fedha hizo zililipwa kihalali kabisa kwa IPTL kutokana na mauzo ya umeme kwa Tanesco.

“Iweje wanasiasa wahoji tu fedha hizo zilizolipwa kwa IPTL kihalali kulipia umeme ambao IPTL ilizalisha na kuiuzia TANESCO na kusambazwa kwa wananchi? Kwani IPTL ni mali ya umma? Je, ilitaifishwa lini?”, alihoji Bw. Makandege. 

Kwa upende wake Katibu Mkuu wa Chama Cha Kijamii (CCK) Renatus Mwabhi, ambae pia alishiriki katika hafla hiyo, amewataka wananchi kuchambua kwa umakini matamshi ya viongozi kabla ya kuyaamini kwakuwa siyo viongozi wote wanalitakia kheri taifa hili.

Mbali na hilo, katibu huyo wa CCK amewataka wananchi na waumini kuliombea taifa kwani kina kila dalili kuwa matendo yanayoendelea hivi sasa hapa nchini yanaweza kuliingiza taifa katika machafuko yasiyo ya lazima.

Katika harambee hiyo zaidi ya shilingi milioni 30 (Tsh 30,000,000/-) zilikusanywa huku kampuni ya IPTL na PAP wakishirikiana na kampuni ya mawakili ya Bulwarks Associate Advocates wakichanga zaidi ya  shilingi milioni ishirini (Tsh 20,000,000/-) ambazo zitachangia katika maendeleo ya kanisa na kuwezesha kwaya hiyo  kurekodi albam yake mpya yenye ujumbe wa neno la Mungu ili kuwawezesha kutimiza azma yao ya kueneza injili kwa watu wote.

Kwa upande wake, mlezi wa kwaya hiyo ya Patano na kwaya ya Edeni ya Kanisa la Morovian la Mjini Arusha, Bw. Philip Makini ambaye pia ni Afisa Mwandamizi wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), aliwapongeza IPTL/PAP na Bulwarks Associate Advocates kwa msaada waliotoa ambao alisema utawawezesha wanakwaya na Usharika kwa ujumla kufanikisha malengo yao. 


Naye Mwinjilisti wa Kanisa la KKKT Usharika wa Likamba, Bi. Martha Musa Kivuyo, kwa niaba ya wanakwaya na wanausharika wote, aliwashukuru Makampuni hayo kwa mchango wao uliowawezesha kuvuka malengo ya harambee hiyo iliyotazamia kukusanya Shilingi milioni 20 (Tsh 20m/-)

No comments: