




…………………………………………………………….
Kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji jana imeanza ziara ya kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa chini ya Ushirikiano wa Nchi za Bonde la Mto Nile (Nile Basin Initiatives) nchini Sudan.
Lengo la ziara hiyo ni kupata uelewa wa pamoja kuhusu ushirikiano uliopo katika kusimamia na kuendeleza rasilimali za Bonde la Mto Nile kati ya Nchi wanachama, huku Tanzania na Sudan zikiwa ni miongoni mwao.
Katika ziara hiyo Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe ambaye ameambatana na kamati hiyo amesema kwamba, dhumuni kuu la ziara hiyo ni kwenda kuona na kujifunza namna Sudan inavyotumia maji ya Mto Nile kwa ajili ya maendeleo yake kiuchumi katika shughuli za kilimo, ufugaji, utalii na biashara.
“Tanzania inachangia asilimia 28 ya maji ya Mto Nile na ina utajiri mkubwa wa rasilimali hii ya maji, hivyo hatuna budi kujifunza kutoka kwa wenzetu ili nasi tupate ufahamu mzuri na tuweze kupata maendeleo makubwa katika nyanja mbalimbali kupitia rasilimali hii. Na hatua ya kwanza ni kuona wenzetu wa Sudan wanafanya nini mpaka kufikia hatua kubwa waliyopiga leo hii”, alisema Prof. Maghembe.
Ziara hiyo ni mwaliko kutoka nchi ya Sudan na itachukua siku nne, itajumuisha kutembelea Bwawa la Merowe linalotumika kwa ajili ya kuzalisha umeme na shughuli za kilimo cha umwagiliaji, inategemewa kuleta tija kwa maendeleo ya Sekta ya Maji nchini na uchumi kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment