UVCCM, UWT Mbeya watoa matamko kupinga kauli zilizotolewa na Wilbroad Slaa na Mkewe dhidi ya Rais Jakaya Kikwete
Mwenyekiti
wa Uvccm Mkoa wa Mbeya Amani Kajuna alisema Umoja wa Vijana hauko
tayari kufumbia macho matusi anayotukanwa Raisi Kikwete na Dk Slaa
anapokuwa akihutubia wanachama wake jukwaani.
Mwenyekiti
wa Uwt Mkoa wa Mbeya Prisila Mbwaga alisema kama Wanawake wa Chama cha
Mapinduzi hawako tayari kuona matusi yanayotolewa na Mke wa Dk Slaa
Josephine Shumbusho juu ya Mama Salma Kikwete kwamba anachangia kuibomoa
Nchi.Picha na Habari na Joseph Mwaisango
---
UMOJA wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi(UVCCM) na
Umoja wa Wanawake (UWT) wa Chama hicho Mkoa wa Mbeya wametoa matamko makali
kupinga kauli zilizotolewa na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo(CHADEMA) Dk. Wilbroad Slaa pamoja na Mkewe juu ya Raisi Kikwete.
Matamko hayo yalitolewa na Wenyeviti hao
katika Mkutano na Vyombo vya habari uliofanyika katika Ofisi za UVCCM Mkoa wa
Mbeya, ambapo walisema kamwe hawawezi kufumbia macho maneno ya uzushi na
uchonganishi kati ya Serikali na wananchi.
Akisoma tamko Mwenyekiti wa Uvccm Mkoa wa Mbeya
Amani Kajuna alisema Umoja wa Vijana hauko tayari kufumbia macho matusi
anayotukanwa Raisi Kikwete na Dk Slaa anapokuwa akihutubia wanachama wake
jukwaani.
Alisema katika Mkutano alioufanya Mei 12, Mwaka
huu Wilayani Mbozi Mkoa wa Mbeya Dk. Slaa akihutubia wananchi kuwa Raisi
Kikwete ni Freemason, Mdini, Mawaziri hawamsaidii pia ni Mafisadi na
kuongeza kuwa ana ushahidi wa Cd ambazo Raisi Kikwete akihamasisha udini
na kuhusu uchinjaji.
Alisema maneno ya Dk. Slaa ni uzushi ambao
unalengo la kufitinisha Watanzania na Serikali ya Chama cha Mapinduzi hususani
anapofanya mikutano ya Hadhara katika Mkoa wa Mbeya ambapo aliongeza kuwa
Ufisadi anaousema yeye kwa Mawaziri wa Ccm ili hali yeye mwenyewe anaongoza kwa
ubadhilifu wa fedha za Wananchi.
Alitolea mfano wa ubadhilifu uliofanywa na
Chadema mkoani Mbeya kuwa ni pamoja na Kitendo chaMwenyekiti wao Freemani Mbowe
kuchangisha fedha Milioni Tatu kwa wananchi kwa kile alichodai zingetumika
kununulia maji na matibabu wakati wa maandamano lakini hazikufanya kazi hiyo na
hazijulikani zilipo.
Kajuna alisema mbali na fedha hizo
kutokujulikana matumizi yake pia Dk. Slaa alichangisha fedha zingine
Shilingi Laki saba kwa ajili ya posho ya Wabunge waliofukuzwa bungeni jambo
ambalo lilileta sintofahamu kwa wakazi wa Jiji la Mbeya.
Alisema ufisadi mkubwa uliopo ndani ya Chadema
ambao kila Mwezi wanapata ruzuku ya takribani Milion mia Tatu lakini hawajawahi
kujenga hata chumba kimoja cha Zahanati wala kutoa msaada kwa wananchi wasiojiweza
lakini wao wanazidi kuwachangisha wananchi.
“ Jamani watanzania fungukeni muone huyu
kiongozi wa namna gani Mlafi, Mchoyo na mchochezi asiyependa kuona amani
ya Nchi ikistawi” alisema Kajuna.
Aliongeza kuwa pamoja na Chadema kupata fedha
zote hizo bado zinaishia mikononi mwa watu wachache hususani Dar Es Salaam
ambapo Mikoani hawazipati na ndiyo sababu Ofisi za Chadema Mkoa wa Mbeya
zilifungwa kutokana na kutolipia pango la Nyumba deni la Shilingi Laki tatu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Uwt Prisila Mbwaga
alisema kama Wanawake wa Chama cha Mapinduzi hawako tayari kuona matusi
yanayotolewa na Mke wa Dk Slaa Josephine Shumbusho juu ya Mama Salma Kikwete
kwamba anachangia kuibomoa Nchi.
Alisema Shumbusho alinukuliwa akitoa matusi
makubwa dhidi ya Mama Salma katika mkutano wa hadhara uliofanyika Wilayani
Mbozi akisema ameshindwa kumshauri raisi kuhusu uongozi na namna ya kuongoza
nchi.
Aliongeza kuwa katika matusi yake alimtuhumu Mke
wa Raisi kuwa ni Mwanamke Mpumbavu anayeibomoa nchi nyumba yake kwa mikono yake
Mwenyewe kama Biblia inavyosema na kwamba yeye atakuwa tayari kumshauri Dk.
Slaa atakapokuwa Raisi mwaka 2015.
Kutokana na tuhuma hizo Umoja wa Wanawake wa
Chama cha Mapinduzi mkoa wa Mbeya wamemtaka Mke wa Dk. Slaa kuacha tabia ya
kumsema vibaya Mama Salma na akiendelea hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi
yake.
Comments