Sunday, January 03, 2010

Stars tutalinda heshima





TAIFA Stars inashuka dimbani kesho kuikabili Ivory Coast ikiwa na lengo moja tu la kutunza heshima yake kwenye Uwanja wake wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Stars ikiwa na nyota wake watatu wanaocheza soka ya kulipwa Nizar khalfan (Vancouver Whitecaps, Canada), Henry Joseph (kongsvinger, Norway)na Muharami Mohamed (Feroviaro, Msumbiji) watakuwa na kazi ya kulinda heshima ya nchi ya kutofungwa na vigogo kwenye uwanja huo.

Ivory Coast iliyowasili nchini majuzi kikiwa na mastaa wake wote akiwemo Didiee Drogba, Solomon Kalou, Bakari Kone na Yahya Toure itaingia uwanjani ikiwa na malengo yote kuhakikisha wanashinda.

Katika uwanja huo Stars iliweza kulazimisha suluhu na Cameroon, ikatoka sare ya 1-1 na Ghana kabla ya kuifunga New Zealand 2-1 mwaka jana.

Akiuzungumzia mchezo huo kocha Marcio Maximo alisema mchezo utakuwa mgumu, lakini watafanya kama walivyofanya kwenye mechi nyingine zilizopita.

''Mchezo utakuwa mgumu kwa kuwa tunacheza na timu nzuri ambayo iko kwenye nafasi nzuri kwenye orodha ya juu ya fifa, lakini tutacheza kama tulivyocheza na Cameroon, New Zealand na Ghana kuhakikisha tunashinda.

Naye nahodha wa Stars, Shadrack Nsajigwa alisema wanacheza na moja ya timu bora duniani iliyojaa wachezaji wanaojulikana duniani kote, wamekuja hapo kwa ajili ya kujiandaa kwa sababu wanajua kuna kitu watapata kutoka kwetu.

''Ni kweli wenzetu ni wazuri na wanajulikana kwa hivyo tunawaheshimu sana, lakini hatuwaoogopi, mechi itakuwa ngumu tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha tunashinda.''

Baada ya mechi ya Stars timu hiyo ya Ivory Coast itacheza mechi nyingine siku ya Alhamisi dhidi ya Rwanda 'Amavubi'.

Ikiwa chini ya kocha wake mkuu Vahid Halhlhodzic, imepanga kuutumia mchezo huo kama kipimo chao kwa ajili ya mashindano ya CAN nchini Angola kwa vyovyote hawatakubali kuupoteza mchezo huo.Habari hii imeandikwa na Doris Maliyaga.

No comments: