MVUTANO wa tarehe ya mkutano mkuu wa klabu ya Simba inadaiwa ni kutokana na kutokamilika kwa taarifa ya fedha ambayo inatakiwa kuwasilishwa kwa wanachama.
Habari ambazo gazeti hili ilidokezwa jana ni kuwa kumekuwa na misigano hiyo ili viongozi kuanza kutengeneza taarifa hiyo ya miaka mitatu.
Viongozi wa Simba wamependekeza mkutano mkuu kufanyika Januari 16, lakini aliyekuwa Katibu Mwenezi wa klabu hiyo, Said Rubeya akizungumza kwa niaba ya wanachama, alisema mkutano ni Jumapili.
Kamati ya Utendaji chini ya mwenyekiti wake, Hassan Dalali iliyokutana Desemba 29, imepanga kufanya mkutano huo Januari 16.
Rubeya alisema kuwa wanapinga maamuzi ya kamati ya utendaji iliyokutana Desemba 29 na kupanga tarehe ya mkutano mkuu kuwa Januari 16.
Alisema Viongozi wa klabu hiyo wamekuwa wakisogeza mbele siku za kufanya mkutano mkuu ilikukwepa kutoa taarifa ya matumizi na mapato ya klabu hiyo.
Hata hivyo, Dalali alisema jana kuwa wanachojua ni kwamba mkutano mkuu ni Januari 16 kama ulivyopangwa na Kamati ya Utendaji ilipokutana Desemba 29, mwaka jana.
Naye Sweetbert Lukonge anaripoti kuwa kamati ya kurekebisha katiba ya uchaguzi ya Simba inakutana leo chini ya Makamu Mwenyekiti Omari Gumbo, Mohamed Mjenga, Hassan Othman ' Hassanoo' na Ayoub Semvua na kupitia marekebisho hayo..
Afisa habari wa klabu hiyo, Clifod Ndimbo amesema kuwa mara baada ya kupitia mapendekezo hayo itayawasilisha katika mkutano mkuu wa klabu wa Januari 16. Imeandaliwa na Clara Alphonce.
Comments