Monday, January 11, 2010

Kisumo awavaa kina Malecela



*ADAI ATAKA WASIGOMBEE UBUNGE, WAWAACHIE VIJANA

MWANASIASA mkongwe nchini, Peter Kisumo amewataka wabunge wenye umri mkubwa kutogombea nafasi hizo katika Uchaguzi Mkuu ujao na badala yake wawaachie nafasi hizo wagombea vijana.

Kisumo ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa CCM aliwahi kutoa kauli kama hiyo mwaka 2005 alipomsindikiza Rais Jakaya Kikwete kutangaza nia yake ya kugombea urais.

Kauli ya Kisumo mwaka 2005 iliibua malumbano na baadhi ya wagombea akiwemo John Malecela aliyelazimika kujibu mapigo kwa kusema hata kama ni mzee, lakini akili yake inakata kama wembe.

Lakini jana Kisumo alirejea kauli hiyo lakini safari hii akiwalenga wabunge na madiwani, wakati akipokea hati ya utambulisho ya kamanda mpya wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilaya ya Mwanga, Seleman Mfinanga.

“Ni matumaini yangu kuwa safari hii wabunge wazee watawaachia vijana kwa kusema hivyo sina maana wazee hawa hawana kazi ya kufanya, wao watabaki kuwa washauri kwa vijana,”alisema Kisumo.

Kisumo aliwataka wabunge na madiwani wazee ambao wameshikilia nyadhifa hizo kwa miaka mingi wasione nongwa kuwaachia vijana akisisitiza kutokana na mabadiliko ya sasa, kunahitajika damu changa.

Mwenyekiti huyo wa Baraza la Wadhamini wa CCM ambaye pia ni Kamanda wa UVCCM Mkoa Kilimanjaro, alisema wapo vijana ambao wamejifunza uongozi na wana sifa za kuiongoza nchi kwa uadilifu mkubwa.

Aliwapongeza Mbunge wa Kwela, Chrisant Mzindakaya na Paul Kimiti wa Sumbawanga kuamua kwa hiyari yao kutogombea tena ubunge akisema wameonyesha mfano na akawataka wengine kuiga mfano huo.

Katika Bunge la sasa, wakongwe wengine ni akina John Malecela, Samwel Sitta na Jackson Makwetta.

Kisumo ametumia nafasi hiyo kukemea kile alichosema kuanza kwa kampeni zinazoegemea katika udini wilayani Mwanga huku akiwataka wananchi kuwa macho na wagombea wa aina hiyo kwa kuwa hawafai.

“Kaeni macho, msiruhusu mtu yeyote kuwachonganisha hapo Mwanga kwa udini kwamba ooh mgombea wa dini fulani ndiye anayefaa kuwa mbunge, mtu wa iana hii ni mchochezi wa vurugu,”alisisitiza.

Mwanasiasa huyo alikemea pia kampeni za ukabila katika jimbo hilo ambapo wagombea ubunge hutambulishwa kwamba ama anatoka Usangi,Ugweno au Tambarare akisema hiyo sio sifa ya uongozi.

Kisumo alifichua kile alichodai kuundwa kwa mabaraza ya wazee wa CCM katika tarafa mbalimbali za jimbo hilo akisema mabaraza hayo yanaundwa ili kutumika katika kampeni na hayako kikatiba.

Kwa upande wake,Mfinanga ambaye alifuatana na Mwenyekiti mpya wa Chipukizi wilaya ya Mwanga, Zena Salim alisema changamoto kubwa inayomkabili kwa sasa ni kupanua wigo wa ajira kwa vijana.

Mfinanga ameteuliwa kushika wadhifa wa Ukamanda wa UVCCM Wilaya ya Mwanga baada ya Cleopa Msuya aliyeshikilia nafasi hiyo kwa miaka zaidi ya 10 kuamua kung’atuka kwa hiyari. Imeandikwa na Daniel Mjema, Moshi.

No comments: