Rais Kikwete amtumia Drogba kupaisha soka Bongo





Rais Jakaya Kikwete akimkabidhi jezi ya timu ya Taifa Stars mcheza ji wa Ivory Coast, Didier Drogba wakati wa hafla ya Chakula cha mchana iliyoandaliwa na Rais kwa wachezaji na viongozi wa Ivory Coast, Rwanda na Taifa Stars iliyofanyika kwenye Hoteli ya Golden Tulip jijini Dar es Salaam jana. Picha na Fidelis Felix

RAIS Jakaya Kikwete amesema kuwa mshambuliaji nyota was Chelsea, Didier Drogba na timu yake ya Ivory Coast watakuwa mabalozi wazuri wa Tanzania baada ya kuweka kambi ya siku sita kujianda kwa fainali za Afrika.

Kikwete alisema hayo wakati alipoiandalia chakula cha mchana timu hiyo inayopewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CAN) kwenye fainali zinazoanza Jumapili nchini Angola.

Akizungumza kwenye hafla hiyo jana, Kikwete alisema kuwa ujio wa timu hiyo iliyosheheni wanasoka nyota wanaosakata soka barani Ulaya utasaidia sana kulitangaza jina la Tanzania na kuwataka nyota hao kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa nchi hii.

"Kwa mfano juzi tuliona kwa mara ya kwanza kituo cha televisheni cha Sky cha Uingereza kilimuhoji Drogba baada ya mechi na Taifa Stars," alisema Kikwete. "Kizuri zaidi alikuwa akizungumzia mambo mazuri kuhusu Tanzania.

"(Drogba) alizungumzia jinsi mechi ilivyokuwa ngumu na jinsi timu yetu (Taifa Stars) ilivyochezavizuri. Alisema alishangazwa kwa jinsi Tanzania ilivyoamua kushambulia badala ya kukaa nyuma kupunguza magoli. Hiki ni kitu kizuri."

Kikwete alisema hayo katika chakula cha mchana alichowaandaliwa wachezaji wa Ivory Coast, Stars na Rwanda iliyofanyika katika hoteli ya Golden Tulip Jijini Dar es Salaam.

Alisema kuwa ujio wa timu hiyo hapa nchini umefanya dunia nzima kujua kuwa Ivory Coast wapo Tanzania na kutaka kufahamu wanafanya nini.

'' Kwa mara ya kwanza nimeona katika kituo cha televisheni cha Sky News maojiano ya Drogba juzi baada ya mechi kuisha hiyo saizi Dunia nzima inataka kujua mchezaji huyo yupo Tanzania na anafanya nini kwa kuwa

Kikwete alisema kuwa Watanzania watajitaidi kuiombea Mungu Ivory Coast na Miungu mingine ili kuhakikisha wanachukua kombe hilo na endapo watafanikiwa kufika fainali za CAN basi Watanzania watakwenda kuwashangilia ili kuakikisha wanakuja na kombe hilo.

Kikwete ambaye aliwakabidhi wachezaji wa Ivory Coast jezi za Tanzania zenye majina yao, aliipongeza serikali ya Ivory Coast na viongozi wa soka wa nchi hiyo kwa kuichagua Tanzania kuweka kambi kujiandaa na michuano hiyo.

Rais wa Shirikisho la Soka Ivory Coast, Jacques Onouma aliipongeza Tanzania kwa mapokezi mazuri walioyapata na ukarimu kutoka kwa wananchi wake hivyo na kuahidi kulileta kombe hilo la CAN na kulipeleka katika Mlima Kilimanjaro endapo watalitwaa. Imeandikwa na Clara Alphonce.

Comments