Membe aonya wakwepa kodi





WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amesema umefika wakati wa mabenki kushirikiana na serikali kudhibiti wafanyabiashara wakubwa ambao wanakwepa kulipa kodi na kuikosesha nchi mapato.

Membe alisema hayo wakati akizindua mpango wa benki ya CRDB wa kuhamasisha matumizi ya kadi za viza na Tembo katika manunuzi jana.

Waziri huyo alisema serikali iko tayari kushirikiana na mabenki kuwezesha utaratibu huo kutumiwa na wafanyabiashara wote.

Membe alifafanua kwamba kuwepo kwa mfumo huo unaotumia teknolojia ya kisasa katika mambo yote ya manunuzi kutoka kwa wananchi kwenda kwa wafanyabiashara, kutapunguza tatizo la ukwepaji kodi nchini, utapeli na ulanguzi.

"Utaratibu mliozindua umeweza kuiunganisha Tanzania na dunia," alisema. "Utaratibu huu hutumika sehemu nyingi duniani, sisi serikali tunachoweza kufanya kushirikiana nanyi ni kuhakikisha wafanyabiashara wanatumia mfumo huu.

"Najua wanaweza kukataa lakini ni wajibu wa serikali kuhakikisha uamuzi huo unatekelezwa kwa kuwa utawezesha kupatikana mapato sahihi na kupunguza ukwepaji kodi. Tunataka wao wanufaike na serikali inufaike kwa mapato."

Katika tukio hilo, Membe alitaka benki nchini kusaidia serikali kuimarisha usalama wa fedha za raia.

Aliongeza kwamba, kwa kawaida kiwango cha uhalifu kinapokuwa juu, wananchi huweza kupoteza imani kwa serikali yao hivyo akataka benki kusaidia kupunguza tatizo hilo katika mzunguuko wa fedha. Imeandikwa na Ramadhan Semtawa.

Comments