Msafara wa Rais wapata ajali

GARI la polisi lililoongoza msafara wa Rais Jakaya Kikwete aliyepo mkoani Shinyanga kwa ziara ya kikazi ya siku tatu jana hiyo liliacha njia na kupinduka na kujeruhi askari.

Walioshuhudia ajali hiyo walisema waliliona gari hilo lililokuwa mbele ya msafara wa rais likiyumba na baadaye kuacha njia na kupinduka kando ya barabara iendayo Meatu. Ajali hiyo ilitokea saa 11 na dakika kumi jioni.

Katika ajali hiyo askari sita walijeruhiwa na ilitokea katika kijiji cha Nyikoboko wakati msafara ukitokea Kisese wakati Rais Kikwete akitoka kuzindua mto Simiyu unaounganisha Wilaya za Bariadi na Meatu.

Walioshuhudia walisema kuwa ajali hiyo ilisababishwa na mvua zilizonyesha na kusababisha utelezi hali iliyosababisha gari la polisi lenye nambari za usajili PT 7414 kuacha njia na askari wawili kujeruhiwa ambao ni Marko Mbambwe na DC Tegemeo. Meya wa mji wa Shinyanga Hassan Mwendapole alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo.

Majeruhi hao wapo katika hospitali ya Wilaya ya Meatu na kwamba katika ajali hiyo gari aina ya Suzuki ambayo ilikuwa karibu na gari iliyopata ajali iligongana na gari iliyokuwa nyuma.

Comments