Thursday, January 28, 2010

Dk Njelekela apata tuzo ya Martin Luther King



MWENYEKITI wa Chama cha Madaktari Wanawake (Mewata), Dk Marina Njelekela amepewa tuzo ya amani ya Dk Martin Luther King l kutokana na kuendesha kwa mafanikio kamapeni ya kupima na kutibu saratani ya matiti na uzazi bure.
Akitoa tuzo hiyo ya 2010 Martin Luther King Jr./ Drum Major for Justice jana kwenye ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam, Balozi Alfonso E Lenhart alisema Dk Njelekela amepata tuzo hiyo kutokana na kupigania utu wa mwanamke kwa kuendesha kampeni hiyo na kuokoa maisha ya kina mama wengi nchini bila kujali kipato chao, elimu wala mahali wanapoishi.
Alisema Dk Njelejela aliafanya kazi kubwa sana kwa kuwa kati ya wanawake 1000 wanaojifungua nchini, sita kati yao hufariki.
Alisema mchango alioutoa Dk Njelekela ulilenga kuweka usawa na utu kwa wanawake, na kuwa hilo ndilo lililokuwa lengo la Dk Martin Luther King, ambaye alikuwa mpigania haki za wanyonge na hasa watu weusi nchini Marekani.
Alisema Marekani itaendelea kushirikiana na Tanzania pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali kama Mewata katika kuchangia sekta ya afya nchini ili kuhakikisha kuwa watu wote bila kujali hali zao za kipato, elimu, wala mahali wanapoishi wanapata huduma bora na sawa za afya.
Akizungumza baada ya kuipokea tuzo hiyo, Dk Njelekela, ambaye pia ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tiba Muhimbili (Muhas), aliishukuru Marekani kwa kutambua mchango wake na kumpatia tuzo hiyo ya amani na kuwataka madaktari nchini kuchukulia tuzo hiyo kama changamoto ya kupigania kuinua na kuboresha afya nchini.
“Kampeni hii kupima na kutibu saratani ya matiti na shingo ya uzazi tuliifanya katika mikoa saba, mimi na wenzangu wa mewata tuliwafikia wanawake kama 64,000,” alisema Dk Njelekela.
Dk Njelekela pia alitumia nafasi hiyo kuiomba Marekani kuiunganisha Mewata na madaktari wengine wa nchi hiyo ili waweze kuendelea kutoa huduma za afya kwa Watanzania.
Mbali na Dk Njelekela watu wengine ambao walishapata tuzo hiyo ni pamoja na Joseph Sinde Warioba (1999), Mwalimu Julius Nyerere (2000), Francis Nyalali (2002), Profesa Godfrey R.V. Mmari (2003) Mama Justa Mwaituka (2004), Balozi Gertrude Mongella (2005), Dk Salim Ahmed Salim (2006), Rashid Mfaume Kawawa (2007), Regnad Abraham Mengi (2008) na jumuiya ya maalibino Tanzania (2009). Imeandikwa na Fredy Azzah.

No comments: