Waweka kambi porini kumpokea Yesu

*Wadai wanamtarajia kushuka nchini kabla ya Machi 30
*Wauza nyumba, mali na kutelekeza jamaa zao
*Serikali yaingilia kati mchungaji akubali kuvunja kambi

Na Richard Kilumbo, Kyela

WAUMINI wa Kanisa la Wasabato wenye imani kali wilayani hapa, wamekimbia makazi yao na kwenda kuweka kambi porini kwa lengo la kujiandaa kumpokea Yesu.

Waumini hao ambao wengine wemetangaza kuuza nyumba na kuwatelekeza ndugu na jamaa zao waliokuwa wakiishi nao, wanaamini kuwa Yesu anatarajia kushuka nchini kabla ya Machi 30, mwaka huu.

Baadhi ya wanafunzi walioathirika na kukimbiwa kwa ndugu na jamaa zao na kuwaacha wakiteseka kwa kukosa mahitaji muhimu, walilieleza Mwananchi kwamba, waumini hao, walianza kuondoka katika nyumba zao wiki iliyopita baada ya ujio wa Mchungaji mmoja kutoka Musoma mkoani Mara, anayedaiwa kuwa Nabii na kuwahamasisha wafanye maandalizi ya kupokea ujio wa Yesu.

Wanafunzi hao ambao waliomba majina yao yahifadhiwe, walisema ndugu hao wamekimbia makazi na kubeba magodoro huku wakiwaacha wao katika nyumba zao bila msaada wowote.

Walisema wengine wamekuwa wakitangaza kuuza mali zao na nyumba na kwenda kuishi katika pori kubwa lililopo katika Kijiji cha Tenende, wakiamia mahali hapo ndipo patakatifu, ambako Yesu atawashukia.

Mwandishi wa habari hizi juzi na jana alitembelea katika Kijiji hicho cha Tenende na kufanya mazungumzo na baadhi ya watu wanaoishi maeneo jirani na waumini hao.

Wakazi hao, walimweleza kuwa, wamekuwa wakiwashuhudia waumini hao, wakiishi katika pori hilo huku wakikesha kwa kufanya maombi ya mara kwa mara.

Mmmoja wa wakazi hao, Job Anyengenye, alisema hashangai kutokea kwa hali hiyo hivi sasa kutokana na watu wengi kutafsiri biblia wanavyoweza na kutumia kifungu kimoja kama wanavyotaka na kusababisha upotoshaji mkubwa wa imani miongoni mwa jamii.

Alisema kinachomkera zaidi ni pale anapoona watoto wadogo wakiteseka kwa kukosa masomo na wengine wakijikuta wanakwenda umbali mrefu kufuata shule wanazosoma kutokana na wazazi wao, kuhamia porini.


Mzee wa Kanisa la Sabato lililopo Kijiji cha Tenende, Jerad Jackson, alisema kundi hilo ni  la waumini waliojitenga kutoka katika Kanisa mama lililopo mjini.

Alidai kuwa, kanisa hilo, uhusiano kabisa na Kanisa Kuu la Kisabato lenye makao makuu yake, mjini Kyela.

Alisema waumini hao wanaendesha huduma yao kwa kufuata misingi na imani zao, wanazozijua.

Baadhi ya Wasabato, wenye imani kali walipotakiwa kuzungumza juu ya uamuzi wao wa kuimbilia porini, walikana kwa madai kuwa sio wasemaji.

Walisema viongozi wao ambao ndio wazungumzaji hawapo.

Hata hivyo, mmoja wao, alisikika hakisema  Yesu hawezi kuja mjini ambako kumekuwa na msongamano mkubwa wa nyumba, nyingi zikiwa zinatumika kwa biashara chafu ambazo ni chukizo kwake.

Alisema ndio maana wameamua kwenda porini ambako ni mahali patakatifu Yesu atakaposhukia.

Taarifa zaidi kutoka kwa baadhi ya waumini hao zinaeleza kwamba viongozi wakuu wote waandamizi katika Kanisa hilo, ambao ni wachungaji  wamesafiri kwenda katika mikoa ya Lindi, Mtwara Tanga na Morogoro kwa ajili ya kuwahamasisha watu waachane na mambo ya dunia na kuuza kila kitu ili washiriki katika ujio wa Yesu.

Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Mashimba Hussein Mashimba amekiri kupata tetesi juu ya waumini hao kuweka kambi porini.

Alisema Serikali inalifanyia kazi suala hilo ili kujua athari zinazoweza kutokea kufuatia uamuzi huo na kutoa uamuzi baadaye.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Suleiman Kova alikiri kusikia taarifa za waumini hao.

Kova alisema kikao cha Ulinzi na Usalama, imekaa na mchungaji huyo, ambaye amekubali kuwarejesha waumini wote katika makazi yao.

"Tumezipata taarifa za hili kanisa na kikao kilichomalizika muda mfupi uliopita kimeamua kwamba waumini wote waliokimbia makazi yao warejee kwao na yeyote atakayekiuka atashitakiwa, " alionya Kamanda huyo.


Alisema kanisa hilo halina usajili na wala halitambuliki na mamlaka zozote halali nchini, hivyo wamemtaka mchungaji huyo, kufuata sheria za nchi kama zinavyoagizwa na kukubali.

Alisema kitendo cha wao (wachungaji) kukikuka taratibu ni kosa kisheria na linashtakiwa chini ya sheria ya kuwakosesha wanafunzi masomo.

Comments