Mufti apelekwa India kutibiwa

Na Mussa Juma, Arusha

HATIMAYE Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa bin Shaban Simba ameondoka kwenda nchini India kwa matibabu ya ugonjwa wa kisukari.

Mufti Simba aliondoka jana majira ya saa 11 jioni Arusha kuelekea nchini India kwa matibabu zaidi baada ya kulazwa kwa zaidi ya wiki mbili.

Mufti (71) aliondoka na ndege ya Shirika la Ethiopia Airline na atapowasili Mumbai India, atapokewa na gari maalum la wagonjwa kuelekea Hospitali ya Jaslok and Research Center ya Mumbai kuanza matibabu.

Katika msafara huo, Mufti ambaye hivi sasa hawezi kutembea akisumbuliwa sana na mguu wake wa kulia ambao umevimba, ameongozana na Daktari wake, Dk Peter Mhando na Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu nchini (BAKWATA) Mkoa wa Arusha, Ally Mzee ambaye pia ni ndugu yake.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, katika hospitali ya KAM – Medical Center , Mufti Simba alisema anakwenda kupatiwa matibabu zaidi katika hospitali hiyo.

Alisema kwa miaka 21, amekuwa akisumbuliwa na ugonjwa huo wa kisukari na kwamba hali yake, ilikuwa mbaya zaidi baada ya kuvimba mguu wake wa kulia.

Comments