Friday, March 14, 2008

Hatimaye wasafiri reli ya kati waondoka Dodoma





Jackson Odoyo na Kizitto Noya wa Mwananchi

KAMPUNI ya Reli Tanzania (TRL) imekubali kuwalipa wafanyakazi wake kima cha chini cha Sh200,000 kwa mwezi baada ya kushinikizwa na serikali na mgomo wa wafanyakazi hao.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu, Omary Chambo alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa serikali imeamua kuingilia kati suala hilo ili kuwanusuru wasafiri wa gari moshi waliokuwa wamekwama Dodoma na Tabora.

Alisema mgogoro kati ya wafanyakazi hao na uongozi wa TRL ulianza siku tano zilizopita na baada ya majadiliano ya muda mrefu kati ya Chama Cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania (Trawu), uongozi wa TRL na serikali.

Alifahamisha kuwa TRL imekubali kuwalipa wafanyakazi hao kwa mujibu wa madai yao kwa kuanzia kima cha Sh160,000 kuanzia mwishoni mwa mwezi na ifikapo Sh200,000 ifikapo Agosti, mwaka huu.

"Mazungumzo yetu na,Trawu, TRL yalidumu kwa siku tatu na Mkurugenzi wa TRL amekubali kuwalipa Sh160,000 kuanzia Machi na ifikapo Agosti mwaka huu ataanza kuwalipa kima kipya cha chini cha Sh200,000 kwa mwezi," alisema Chambo. (Picha zote za Michael Uledi)

No comments: