Barua ya Wazi ya Ras Bush kwa Watanzania

Wananchi wapendwa wa Tanzania:

Laura na mimi tunapenda kuwashukuru sana kwa kutukaribisha katika nchi
yenu nzuri wiki chache zilizopita.


Tanzania inafahamika kwa ukarimu wake mkubwa, na ziara yetu
inathibitisha kuwa kweli mnastahili sifa hiyo! Kuanzia maelfu ya
wananchi mliojipanga barabarani kutukaribisha, hadi kwa watoto walioimba
na kucheza kwenye sehemu mbalimbali kama vile Ukumbi wa Karimjee,
Taasisi ya WAMA, pamoja na Shule ya Wasichana wa Kimasai kule Arusha,
kwa kweli mmegusa mioyo yetu sana!

Ninajua kwamba, kuwa mwenyeji wa ugeni wa Rais ni jukumu kubwa, na
ninatambua kwamba kulikuwa na wakati ambapo ziara yetu ilileta matatizo
ya usafiri, pamoja na usumbufu mwingine. Napenda kuwashukuru sana nyote
kwa uvumilivu wenu wakati wa ziara yetu.

Kama mnavyojua, hii ilikuwa ni ziara rasmi ya kwanza kufanywa na Rais wa
Marekani aliye madarakani. Ziara hii si tu kwamba ilikuwa na tija na
mafanikio kwa upande wa mazungumzo ya serikali-kwa-serikali, bali pia
ilikuwa ni fursa muhimu kwa Wamarekani wa kawaida kujifunza mengi kuhusu
taifa lenu. Kupitia picha zilizopelekwa Marekani, waliweza kuona nchi
inayopendeza iliyojaa watu wazuri.

Waliona Watanzania wa ngazi zote wakifanya kazi kwa bidii kujenga mustakabali bora wenye mafanikio mazuri. Waliona vijana waliodhamiria kuendeleza dira ya Mwalimu Nyerere ya kujenga Tanzania yenye amani na umoja.

Niko tayari kuendelea kufanya kazi na Rais Kikwete pamoja na viongozi
wengine, kuisaidia Tanzania kushughulikia changamoto zinazoikabili.
Tunashukuru kwa urafiki wake na urafiki wenu, na tutaendelea kutoa
misaada yetu, wakati mnapozidi kusonga mbele.

Ni matumaini yangu kwamba Laura na mimi tutawatembelea tena katika miaka
ijayo. Mpaka wakati huo, asanteni tena kwa urafiki na ukarimu wenu.
Asanteni sana!

Wenu,

Rais George W. Bush

Marekani


Comments

Love the photos. The title photo is beautiful.
thanx sir. I have paid visit on your site its really good