TRL yakodisha injini tisa za treni


Na Jackson Odoyo wa Mwananchi

KAMPUNI ya Reli Nchini (TRL) imeingiza injini tisa za gari moshi za kukodi kutoka India.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Narasimhaswami Jayaram alisema injini hizo si mpya bali wamezikodisha kutoka katika kampuni ya reli ya nchi hiyo na zimetumika miaka kumi iliyopita.

Jayaram alisema TRL inalipa kiasi cha dola za Marekani milioni 60 kwa mwaka kwa kukodisha injini hizo ili iweze kutekeleza malengo yake.

“Injini hizo siyo mpya ila ziko katika hali nzuri na bado zitaweza kutumika kwa kipindi kirefu na ni kubwa mara mbili zaidi ya zilizopo."

Hata hivyo alisema kwamba kuwasili kwa injini hizo zitaiwezesha shirika hilo kurahisisha safari za Kanda ya Ziwa inyaounganisha mikoa ya Mwanza na Kigoma.

“Injini hizo ziliwasili nchini tangu Januari 23 mwaka huu na leo zinashushwa kutoka kwenye meli na baada ya kushushwa zitapelekwa moja kwa moja katika karakana ya Morogoro kabla hazijaanza kazi kwa ukaguzi wa kiufundi,” alibainisha. (Picha ya Deus Mhagale)

Comments