SHERIA MPYA YA TAKWIMU KUONGEZA UFANISI WA SHUGHULI ZA KITAFITI NA UPATIKANAJI WA TAKWIMU SAHIHI NCHINI.
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu ujio wa sheria mpya ya Takwimu ya mwaka 2015 iliyopitishwa na Bunge Mwezi Machi mwaka huu leo jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa Ofisi hiyo Bw. Morrice Oyuke.
Wadau mbalimbali na waandishi wa habari wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa wakati akitoa ufafanuzi kuhusu ujio wa sheria mpya ya Takwimu ya mwaka 2015.
………………………………………………………….
Na. Veronica Kazimoto. Dar es salaam.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu imesema kuwa Sheria Mpya ya Takwimu ya mwaka 2015 haina lengo la kuzuia Taasisi au watu binafsi kufanya tafiti zao hapa nchini bali inalenga kuweka misingi imara ya shughuli za kitakwimu na tafiti zenye ulinganifu unaotokana na mfumo rasmi utakaoondoa uwepo wa takwimu zinazokinzana.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa wakati akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu ujio wa sheria hiyo mpya iliyoridhiwa na Bunge Mwezi Machi mwaka huu.
Amesema kuanzishwa kwa sheria hiyo kunalenga kutoa mwongozo kwa Taasisi za Serikali na Mashirika mbalimbali yanayozalisha takwimu hapa nchini ili yaweze kuendesha shughuli za ukusanyaji na usambazaji wa takwimu kwa kuzingatia sheria hiyo mpya na kuwa huru kutoa takwimu sahihi zinazoendana na uhalisia wa Tanzania.
“Sheria hii hailengi kuondoa uhuru wa taasisi nyinine za utafiti zilizopo kisheria kufanya kazi zao, taasisi hizo zitaendelea kuwa huru kufuata taratibu zao ilimradi hazikiuki sheria hii” Amesisitiza Dkt.Chuwa.
Comments