ATCL YAONGEZA SAFARI ZAKE VISIWA VYA COMORO.

Na Mwandishi wetu
………………………………………
Dar es Salaam: May 29, 2015: SHIRIKA la ndege la taifa (ATCL) limetangaza  uamuzi wake wa kuongeza idadi ya safari zake kuelekea visiwa vya Comoro hatua inayolenga kuendana  na ongezeko la mahitaji ya huduma za shirika hilo hususani katika kuelekea kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Kwa sasa shirika hilo linatoa huduma zake kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Kigoma na Mtwara kila siku. Sambamba na kutoa huduma hizo hapa nchini, shirika hilo lina mpango mpya utakaoanza rasmi tarehe mosi ya mwezi Juni mwaka huu kwa kuongeza safari zake kuelekea visiwa vya Comoro hadi kufikia mara nane kwa wiki ikiwemo mara mbili siku za Alhamisi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL Bw. Johnson Mfinanga alisema shirika hilo ndilo pekee linalotoa huduma ya safari za anga kati ya Tanzania na Visiwa vya Comoro huku akibainisha fursa za kibiashara zilizopo kati ya nchi hizi mbili jambo linalosababisha uwepo wa ongezeko la mahitaji ya huduma za ATCL.
Pia amewaasa watanzania hususan wakazi wa mtwara kuchangamkia fursa hizo kwa kuwa shirika hilo kwa sasa linatoa huduma zake kati ya Mtwara na visiwa vya Comoro kwa siku za Jumatano na Ijumaa kila wiki.
“Siku zote tumekuwa tukihakikisha kwamba tunabadilika kuendana na mahitaji ya wateja wetu. Ni dhahiri kwamba katika kipindi hiki kuna hitaji kubwa la usafiri wa anga kuelekea visiwa vya Comoro kwa sababu za  kibiashara, mapumziko na sherehe mbalimbali, hivyo ATCL imejipanga kuchangamkia fursa hiyo,’’ alibainisha.
Akizungumzia ufanisi wa shirika hilo katika safari nyingine ikiwemo zile za Kigoma na Mtwara, Bw. Mfinanga alisema wamekuwa wakihudumia idadi kubwa ya abiria kutokana na ndege za shirika hilo kusafiri kwa mwendo kasi wa kuridhisha sambamba na huduma nzuri zinazotolewa kwa wateja wakati wa safari.
“Zaidi tunaamini kwamba huduma tunazozitoa kati ya Tanzania na Comoro zimekuwa zikichangia kuongeza ushirikiano baina ya nchi hizi mbili na tunaamini kuwa hata hili ongezeko la safari zetu kwenye mataifa haya mawili zitatoa fursa kwa wateja wetu kufaidi fursa zinazopatikana ndani ya nchi hizi,’’ aliongeza Bw. Mfinanga
Kuhusu mpango wa shirika hilo kujipanua zaidi kihuduma, Bw. Mfinanga alisema:  “Ndege yetu aina ya De-Havilland Dash 8 Q300 kwa sasa inafanyiwa marekebisho makubwa kwenye karakana yetu iliyopo kwenye uwanja wa Ndege wa Kimataifa  wa Julius Nyerere (JNIA) na itakapokamilika tutaendelea na huduma zetu katika mikoa ya Mwanza, Tabora, Kilimanjaro na Mbeya,’’
Bw. Mfinanga aliongeza kuwa kwa kufanya safari zake kuelekea visiwa hivyo shirika hilo limekuwa likiwezesha wateja wake kunufaika na fursa zilizopo kwenye visiwa hivyo huku pia akitoa wito kwa watanzania wengine kujitokeza kushiriki katika kuchangamkia fursa hizo.

Comments