Friday, July 11, 2014

SERIKALI KUJENGA UPYA RELI YA KATI – WAZIRI MKUU

1(5)
*Ujenzi kugharimu USD bilioni saba
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali ina mpango wa kujenga reli mpya ya kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza kupitia mikoa na ya kati na kuelekea Isaka hadi Burundi ambayo ujenzi wake utazinduliwa rasmi Desemba, mwaka huu
Ametoa kauli hiyo jana jioni (Alhamisi, Julai 10, 2014) wakati akijibu maswali kutoka kwa Watanzania waishio Reading katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa hoteli ya Crowne Plaza.
Waziri Mkuu ambaye alitumia usafiri wa treni kwenda na kurudi mji wa ​Reading kutoka London, alisema ni mara yake ya kwanza kufika kwenye mji huo na akaahidi katika siku za usoni kufanya mikutano ya aina hiyo kwa Watanzania waishio kwenye miji mingine ya Uingereza kulingana na ratiba ambayo watu wa ubalozini watakuwa wameipanga.
“Kuna mtu ameulizia kuhusu tatizo la usafiri nchini Tanzania, napenda kuwahakikishia kwamba Serikali imeamua kuwekeza kwenye mradi mkubwa wa ujenzi wa reli ya kati. Reli hii itaanzia Dar es Salaam hadi Isaka, Isaka hadi Burundi; itatokea Tabora hadi Kigoma na Tabora hadi Mwanza pamoja na kipande cha Kaliua hadi Mpanda,” alisema.
“Mradi huu ni mkubwa ambao ujenzi wake utagharimu dola za marekani bilioni saba, na utatuchukua karibu miaka minne. Kwa hiyo ikiifika Desemba, mwaka huu utafanyika uzinduzi rasmi kwa njia zote hizi za reli,” alisisitiza Waziri Mkuu.
Alisema ili kufanikisha ujenzi Serikali imeamua kujenga upya reli ya kati kwa standard gaugehaliambayo haitaathiri usafiri wa treni kwa kutumia njia ya zamani. “Safari hii tumeamua kujenga upya, na siyo kubanduabandua ili wakati reli mpya ikiendelea kujengwa na ile ya zamani inaendelea kutoa huduma kama kawaida,” alisema huku akishangiliwa.
Maswali mengine aliyoulizwa Waziri Mkuu yalihusu ujenzi wa barabara ya Lindi-Mtwara, ujenzi wa hospitali ya Kagwa, ujenzi wa uwanja wa ndege wa Musoma, utaratibu wa utoaji wa mizigo bandarini na usumbufu wanaoupata, uraia wa nchi mbili, tatizo la walimu na hali ya elimu nchini ambayo yote aliyajibu na kuahidi kufuatilia masuala mengine akifika nyumbani
Kwa ujumal, Waziri Mkuu aliwataka Watanzania waishio nchi za nje (wana Diaspora) kufuatilia kwa makini mikutano ya uwekezaji (Investors’ Forums) ambayo hufanyika kwa kanda au kwa mikoa ili iwasadie kubaini fursa za uwekezaji zilizoko kwenye mikoa wanayotoka. “Tumieni fursa hizi, zitawasaidieni kubaini kwa haraka ni maeneo gani mnaweza kuwekeza kwa haraka. Kama Diaspora mnaweza pia kutumia kipengele cha utalii wa Tanzania kutusaidia kuitangaza nchi yetu,” alisema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu kesho jioni (Jumamosi, Julai 12, 2014) anatarajiwa kukutana na Watanzania waishio Uingereza kwenye mkutano utakaofanyika kwenye ubalozi wa Tanzania, jijini London.

No comments: