NYOTA ya mwanamitindo wa kimataifa wa Tanzania, Flaviana Matata amezidi kung’ara baada ya kuingia katika orodha ya wanamitindo saba bora kwa upande kipato.
Kwa mujibu wa gazeti la biashara la kimataifa la Forbes kwa bara la Afrika (Forbes Africa) lililotolewa hivi karibuni, Flaviana ni mrembo pekee aliyeingia katika orodha hiyo kwa wanamitindo wa Afrika Mashariki na kuzidi kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania kimataifa.
Katika orodha hiyo, mwanamitindo Maria Borges wa Angola ndiyo aliibuka namba moja na wengine sita pamoja na Flaviana wakibaki kutoa ushindani mkubwa kwa mlimbwende huyo wa Angola.
Mbali ya Flaviana, wanamitindo wengine ambao wapo katika orodha hiyo ni Candice Swaenpoel, Katryn Kruger wote wakitokea Afrika Kusini, Ajak Deng, Grace Bol ( Sudan)na Liya Kebede wa Ethiopia,.
Flaviana Matata aliibuka katika jukwaa la kimataifa kama Miss Universe Tanzania mwaka 2007 na aliweka historia kwa kuingia 10 bora na baada ya kumaliza muda wake aliendelea na fani ya uanamitindo Afrika kusini na baadaye alipata nafasi ya kufanya kazi Marekani na Ulaya katika makampuni makubwa ya uanamitindo ya Next Models International na sasa yuko Wilhelmina Models.
Comments