Tuesday, March 30, 2010

YALIYOJIRI UZINDUZI KITABU CHA SIR GEORGE





Mambo kibao yalijiri wakati Rais Jakaya Kikwete alipozindua kitabu kiitwacho ‘Sir George’ Ijumaa iliyopita kilichoandikwa na mtoto wa Balozi, George Kahama katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam.
Marais wastaafu wa awamu ya pili na ya tatu yaani Alli Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa walikuwapo kwa upana zaidi na wakashiriki katika tukio hilo kwa kina mbali na viongozi hao piwa walikuwapo viongozi maarufu waliopata kuwapo katika awamu zote tangu ya kwanza.
Kitabu hiko kinachoeleza historia ya Tanzania kupitia miaka 50 ya utumishi wa Kahama, kilianza kuandikwa mwaka 2006 na utangulizi wa kitabu hiko umeandikwa na Rais Kikwete.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Kikwete alitoa wito kwa watu wa matabaka mbalimbali kujenga tabia ya kusoma vitabu na kuandika vitabu vinavyohusu masuala mbali mbali nchini.
“Ninafarijika kuzindua kitabu hiki cha Sir George kutokana na ukweli kwamba kitabu hiki kitakuwa cha manufaa kwa taifa letu, kutokana na kueleza historia ya taifa letu kabla na baada ya uhuru na sio kwa familia ya Kahama tu,”alisema.
Akizungumza katika hafla hiyo mwandishi wa kitabu hiko Joseph Kahama alisema kuwa kitabu hiko kinachambua mahusiano ya kiuchumi baina ya Tanzania na nchi rafiki hususani Jamhuri ya watu wa China.
“Imani yangu baada ya kuwa karibu na China na kuelewa mifumo yao ya kiuchumi na matumizi ya rasilimali katika kukuza uchumi, Tanzania inaweza kufikia hali ya uchumi wa nchi ya maendeleo ya kati,”alisema.
Hata hivyo balozi George Kahama alikiri kuwa kuna baadhi ya mambo ambayo akiwa mtumishi alishindwa kuyafanikisha, aliyataja mambo hayo kuwa ni ujenzi wa makao makuu ya taifa Dodoma.
Pili ni kuanzishwa kwa benki ya ushirika alisema akiwa waziri wa Ushirika na Masoko 2000-2005, alidhamiria kuanzisha benki ya ushirika ambayo ingeshirikisha Saccos zote nchini kama wanahisa wakuu.
Mwisho ni ndoto ya Zanzibar akiwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa hoteli za serikali ya Zanzibar, alifahamu vizuri mandhari na utajiri wa Zanzibar ambao ukitumiwa vizuri unaweza kuinua uchumi wa Tanzania na kuitangaza vyema sekta ya utalii nchini..Imeandikwa na UMMY MUYA. SOURCE: MWANANCHI.

No comments: