Monday, March 22, 2010

Waijua mibono kaburi



SERIKALI wilayani Kisarawe, imewahakikishia wananchi wa vijiji 11 wilayani Kisarawe ambao ardhi yao imemilikishwa kwa mwekezaji wa zao la Jatropha wilayani humo, kampuni ya Sun Biofuel ya Uingereza, watalipwa fidia zao baada ya uchambuzi yakinifu.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Hanifa Karamagi, mara baada ya kufanya ziara ya kukagua mradi huo, unaomilikiwa na mwekezaji huyo, ambayo inafanya mradi wa kilimo cha zao la Jatropha, au jina maarufu la mibono kaburi, kwa lengo la kuzalisha mafuta ya dizeli.

Karamagi alisema, kampuni hiyo ya uwekezaji toka nchini Uingereza, ilifuata sheria, taratibu na kanuni zote za uwekezaji na umilikaji ardhi ya vijiji kwa mujibu ya Sheria ya Ardhi ya Vijiji Namba 5 ya Mwaka 1999, ikiwemo kulipa fidia stahiki kwa vijiji husika, hivyo serikali inafanya uchambuzi yakinifu kubaini kama kuna wanavijiji wowote ambao hawakupata malipo ya fidia zao kwa namna moja ama nyingine.

Karamagi pia alitoa pongezi kwa mwekezaji huyo kwa kutoa ajira rasmi zaidi ya 400 kwa wanavijiji wa vijiji vinavyozunguka mradi huo ikiwa ni pamoja na kuwalipia mafao NSSF, na kusema ajira hizo zitaboresha maisha ya wanavijiji hao, na akawasisitiza wanavijiji hao, wasibweteke na fedha za mishahara kwa kufanyia starehe, kulewa na kuongeza idadi ya wanawake, bali wazitumie fedha hizo kuboresha maisha yao na kujiletea maendeleo, ikiwemo kuendeleza kilimo cha mazao ya chakula huko vijijini kwao.

Katika ziara hiyo, Mkuu huyo wa wilaya aliyekuwa amefuatana na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Kisarawe, alijionea takriban hekari 1,000 ambazo zimeshalimwa na kupandwa zao hilo, ikiwemo kushuhudia baadhi ya miche ambayo tayari imeshazaa matunda hayo ambayo mbegu zake hutumika kuzalisha mafuta ya dizeli ambayo ni rafiki wa mazingira.

Akimkaribisha mkuu wa wilaya, Meneja wa Kampuni hiyo ya Sun Biofuel nchini Tanzania, Peter Auge, alisema, kati ya ekari 8200 ambazo kampuni yake imemilikishwa, ni 6,000 tuu ndizo zitatumika kwa kwa kilimo cha mibono na eneo lililobakia litatumika kama eneo la hifadhi ya misitu asilia. Pia kampuni hiyo, itaongeza ajira toka 400 zilizopo sasa mpaka 1500 katika kipindi cha miaka mine ijayo.

Vijiji vya Mtamba, Muhaga, Marumbo, Paraka, Kidugalo, Kului, Mtakayo, Vilabwa, Mitengwe, Mzenga ‘A’ na Chakaye ndivyo wafaidika wakuu wa mradi huo, ambapo licha ya wanavijiji hao kupa ajira za moja kwa moja, kwenye mradi huo, mwekezaji huyo wa Sun Biofuel, atawajibika kuboresha huduma za jamii ukiwemo upatikanaji wa maji safi na salama, na kuchangia huduma mbalimbali za maendeleo ikiwemo miradi ya afya na elimu.

Kampuni ya Sun Biofuel (T) Ltd, inamilikiwa kwa ubia kati ya Watanzania na Waingereza ambapo imejikita katika kilimo cha zao hilo la Jatropha kwa jina maarufu la Mibono Kaburi ambalo hustawi kwenye ardhi kame na isiofaa kwa kilimo cha mazao ya chakula.
SOURCE:MWANANCHI

No comments: