Friday, March 26, 2010

Mamia ya miti yapandikizwa Dar




Mkurugenzi Mtendaji wa Zain Tanzania Khaled Muhtadi (kushoto) akipanda mti kuazimisha siku ya utunzaji wa mazingira jana jijini Dar es Salaam. Kampeni hiyo imeendeshwa na Shirika la linalojishugulisha na shuguli za utunzaji wa mazingira na mimea la WWF kwa kushirikiana na Zain Tanzania. Kulia ni Meneja Uhusiano wa Zain Tanzania Muganyizi Mutta.

======================================

MAMIA ya miti imepandwa katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam katika zoezi lililofanywa na kampuni ya simu za mikononi nchini Zain Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Hifadhi ya Mazingira na Mali hai zingine (WWF) pamoja na Manispaa ya Kinondoni jana walishiriki kazi ya upandaji miti, ili kushiriki saa moja ya kuzima taa katika miji mikubwa duniani.

Saa moja ya kuzima taa huadhimishwa Machi 27 ya kila mwaka kwa nia ya kuonyesha umuhimu wa kupunguza hewa ya ukaa na uhifadhi wa mazingira na kutoa elimu juu ya athari ya uharibifu wa mazingira kwa binadamu.

“Kampeni hii ilianza rasmi mwaka 2007 nchini Australia hadi sasa ikiwa inatarajia kupata nchi washiriki zaidi ya 120 ukilinganisha na miji 88 iliyonga mkono suala hili hapo awali;

“Zoezi hili huenda sambamba na kuzima taa kwa muda wa saa nzima kuanzia saa 2.30 usiku tarehe 27 kila mwaka, hufanya hivi kwenye Miji mikubwa ili kuwakumbusha kuwa uhifadhi wa mazingira ni muhimu na kuna haja ya kupunguza joto duniani,”alisema Meneja uhifadhi wa WWF Tanzania Petro Masolwa.

Aliongeza kuwa, kulingana na hali halisi ya umeme Tanzania kuwa ya matatizo wao wameamua kufanya zoezi la upandaji miti badala ya kuzima taa, ili kuikumbusha jamii umuhimu wa kutunza mazingira.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Zain Tanzania Khaled Muhtadi alisema, wadau wa mazingira walioshiriki wameonyesha kuguswa na suala hilo na kuahidi kutoa ushirikiano pamoja na kampuni yake katika kutunza mazingira nchini.

“Tunafurahi kushiriki katika mradi huu, tunawashukuru wadau wa mazingira,Manispaa ya Kidondoni na WWF kuweza kufanya zoezi hili, tutatoa ushirikiano wa karibu ili kutunza mazingira,”alisema Muhtadi.

Mkuu wa Wilaya Kinondoni Jordan Rugimbana aliyasihi makampuni mengine kuiga mfano huo ili kuinusuru nchi kuepukana na mabadiliko ya tabia nchi.

“Kuna haja ya makampuni mengine kuiga mfano huo matokeo ya mafuriko kama yaliyoleta maafa Kilosa na ukame maeneo ya Loriondo ni mabadiliko yenye kuhitaji jitihada za maksudi kuchukuliwa ili kuinusuru nchi yetu,”alisema Rugimbana.

Miti hiyo aina ya Washington Palm ilipandwa katika manispaa ya Kinondoni kuanzia Moroko Mataa hadi Namanga, zoezi hilo likitarajiwa kuendelea katika sehemu nyingine za jiji la Dar es Salaam na nchi nzima. Imeandikwa na Aziza Athuman. SOURCE: MWANANCHI

No comments: