Tuesday, March 09, 2010

Polisi yaomba msaada kumnasa muuaji wa mke wa Balozi Daraja


Balozi Daraja.

Maandalizi nyumbani kwake.
JESHI la Polisi Kanda ya Dar es Salaam limeomba ushirikiano kutoka kwa wananchi ili kusaidia kumkamata mtu anayetuhumiwa kumuua mke wa balozi mwandamizi wa zamani wa Tanzania nchini Marekani, Andrew Daraja.

Anna Daraja, mke wa balozi huyo, aliuawa juzi nyumbani kwake Kimara Temboni kwa kuchomwa kisu kifuani na mtu ambaye anatuhumiwa kuwa ni James Mabakuri, 22, ambaye alikuwa mhudumu wa shamba.

Kaimu kamanda wa polisi wa Kanda ya Dar es Salaam, Charles Kenyera alisema kuwa polisi wamekuwa wakimfuatilia mtuhumiwa tangu tukio hilo litokee lakini hawajafanikiwa kumpata mtuhumiwa.

“Tangu litokee tukio hili la mauaji tumekuwa tukimtafuta mtuhumiwa kwa kuwa yeye alikuwa akiishi katika nyumba ile na baada ya mauaji hakuonekana na hajulikani yuko wapi,” alisema Kenyela.

“Tunaomba wananchi wanaomfahamu kijana huyo pamoja na mwajiri wake kushirikiana na Jeshi la Polisi ili tuweze kumkamata... nasema hivi kwa kuwa polisi hatuwezi kumfahamu bila kuwepo kwa ushirikiano kumpata itakuwa kazi ngumu, tunaamini kuwa malengo yake yalikuwa ya kinyama.”

Kamanda Kenyera alisema kuwa Februari 14 mwaka huu Balozi Daraja alimuaga mke wake kuwa anasafiri kwenda Muheza, Tanga na kumuacha na mhudumu wa shamba ambaye alikuwa akiishi kwenye nyumba hiyo.

“Balozi Daraja aliporejea alifika getini na kugonga geti, lakini hakuna mtu yeyote aliyefungua ndipo dereva wake alipoamua kuruka uzio na kwenda kufungua mlango lakini alipoingia ndani alikuta mwili wa marehemu ukiwa gereji huku kisu kikiwa kimechomwa kwenye titi, mpaka sasa hatujafanikiwa kwa lolote ila tunamshuku huyu kijana kwa nini atoweke baada ya kutokea mauaji,” alisema Kenyela.

Vyombo vya habari jana vilimnukuu kamanda wa polisi wa Kinondoni, Elias Kalinga akisema kuwa baada ya kuhakikisha mama huyo amekufa, mtuhumiwa alifanya upekuzi kwenye nyumba hiyo, ikiwa ni pamoja na chumba cha balozi na kuiba kiasi cha Sh2 milioni na kutoweka kusikojulikana.

Akizungumza na Mwananchi nyumbani kwake, Balozi Daraja alisema kuwa mazishi yatafanyika Ijumaa ya wiki hii Muheza, Tanga na kuongeza kuwa kinachosubiriwa ni mtoto wa marehemu anayesoma nchini Marekani.

“Tunatarajia kuondoka Alhamisi kueleleka Muheza kwa mazishi kwa kuwa kijana wangu atafika kabla ya siku hiyo. Huyu kijana ninamshuku ila siwezi kusema kuwa yeye ndio aliyeua lakini akipatikana na uchunguzi ukafanyika ndio ukweli itajulikana,” alisema Daraja.

Katika hatua nyingine Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, ametuma salamu za rambirambi kwa Balozi Mstaafu Andrew Daraja kufuatia mauaji ya Anna Daraja, yaliyotokea mwishoni mwa wiki.

Taarifa iliyotolewa na Idara ya Mawasiliano Ikulu jana, Rais Kikwete alisema kuwa ameshitushwa na kuhuzunishwa na mauaji ya mama huyo, aliyekuwa na umri wa miaka 65, ambayo alisema mazingira yake hayajafafanuliwa.

“Nimepokea kwa majonzi na huzuni nyingi kifo cha Mama Anna Daraja. Nilipata kumfahamu binafsi Mama Daraja. Alikuwa mtu mwema na mpenda watu.” Amesema Rais Kikwete katika rambirambi hizo na kuongeza:

“Napenda kwa dhati ya moyo wangu kukutumia wewe, ndugu Andrew Daraja pamoja na familia yako yote, ndugu na jamaa zako wote, rambirambi zangu za moyoni kabisa kutokana na kifo hiki cha ghafla.” Habari hii imeandikwa na Fidelis Butahe: SOURCE: MWANANCHI.

1 comment:

Anonymous said...

Genial dispatch and this mail helped me alot in my college assignement. Gratefulness you as your information.