Rais Magufuli atoa siku 7 kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kumaliza deni wanalodaiwa na NHC
Na: Lilian Lundo- Maelezo
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametoa siku 7 kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kulipa deni la bilioni 2 ambalo wanadaiwa na Shirika la nyumba la Taifa (NHC).
Dkt. Magufuli ametoa agizo hilo kwa Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi, Injinia Joseph Nyamhanga leo jijini Dar es Salaam katika ziara ya kushtukiza ya kuangalia ujenzi wa hosteli za wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
“Nawapa siku 7 muwe mmelilipa hilo deni huku mkiendelea na utaratibu wa kuhamia Dodoma, kama hamtalilipa kwa wakati nitawaagiza NHC kuwatolea vitu vyenu nje kama wanavyofanya kwa wengine,” alisema Dkt. Magufuli.
Amesema kuwa kiwango hicho cha bilioni 2 kingeiwezesha wizara hiyo kujenga ofisi za wizara kwa kuwatumia Wakala wa Majengo (TBA) ambao wako chini ya wizara hiyo badala ya kutumika kama kodi ya pango.
Aidha, ameitaka wizara hiyo kuhamia Mjini Dodoma mara tu watakapokamilisha deni hilo na kutoendelea kupanga jijini Dar es Salaam, kwani hakuna sababu ya kuendelea kupanga majengo ya ofisi Dar es Salaam wakati Serikali yote inahamia Dodoma.
Wakati huohuo, Rais Dkt. Magufuli ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Tecknolojia, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na Wakala wa Majengo (TBA) na uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kusimamia vizuri mradi wa ujenzi wa hosteli za chuo kikuu ambao Rais mwenyewe aliahidi shilingi bilioni 10 katika ujenzi huo, bilioni 5 imekwishatolewa na bilioni nyingine 5 itatolewa ndani ya wiki hii.
Hosteli hizo zinategemea kuchukua wanafunzi 4000 ambapo itapunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la wanafunzi kukaa nje ya maeneo ya chuo.
Comments