Tuesday, September 20, 2016

MAABARA YA HOSPITALI YA MNAZIMMOJA ZANZIBAR YAKABIDHIWA CHETI CHA ITHIBATI YA KIMATAIFA


Afisa wa Viwango vya Ubora wa Maabara ya Hospitali Kuu ya Mnazimmoja Muhamed Soud Muhamed akielezea hatua zilizochukuliwa na Maabara hiyo mpaka kufanikiwa kukabidhiwa cheti cha Ithibati ya Kimataifa. 
Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo akibadilishana mawazo na Afisa Mtendaji Mkuu wa SADCAS Maureen Mutasa wakati wa sherehe za kukabidhiwa cheti cha Ithibati ya Kimataifa kwa maabara ya Hospitali ya Mnazimmoja zilizofanyika Hospitalini hapo. 
Afisa Mtendaji Mkuu wa SADCAS Maureen Mutasa akizungumza katika sherehe za kukabidhi cheti cha Ithibati ya Kimataifa kwa ajili ya Maabara ya Hospitali ya Mnazi mmoja. 
Afisa Mtendaji Mkuu wa SADCAS Maureen Mutasa akimkabidhi Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo cheti cha Ithibati ya Kimataifa kwa ajili ya Maabara ya Hospitali ya Mnazimmoja. 
Baadhi ya wafanyakazi wa Wizara ya Afya wakifuatilia sherehe za kukabidhiwa cheti cha Ithibati ya Kimata kwa ajili ya Maabara ya Hospitali Kuu ya Mnazimmoja. 
Baadhi ya wafanyakazi wa Maabara ya Hospitali ya Mnazmmoja wakifurahia vyeti walivyokabidhiwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa SADCAS wakiwa ndani ya maabara yao Hospitali ya Mnazimmoja. 

Picha na Makame Mshenga/Maelezio Zanzibar. 

………………………………………………………… 

Na Ramadhani Ali/Maelezo Zanzibar 

Hospitali Kuu ya Mnazimmoja imepokea cheti cha Ithibati ya Kimataifa kwa ajili ya Maabara ya Hospitali hiyo kutoka Bodi ya Kimataifa ya Ithibati ya Nchi za Ukanda wa Kusini mwa Afrika (SADCAS) katika hafla iliyofanyika Hospitalini hapo. 

Mtendaji Mkuu wa SADCAS Maureen Mutasa alimkabidhi cheti cha Ithibati Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo kutokana na huduma bora zinazotolewa na Maabara hiyo. 

Akitoa maelezo ya kupatikana cheti cha Ithibati ya Kimataifa, Afisa wa viwango vya ubora wa Maabara ya Hospitali Kuu ya Mnazimmoja Mohamed Soud amesema ni mashirikiano ya pamoja kati ya uongozi na wafanyakazi wa maabara, Hospitali Kuu ya Mnazimmoja na Uongozi wa Wizara ya Afya . 

Amesema haikuwa jambo rahisi kufikia hatua hiyo kutokana na changamoto nyingi zilizokuwa zikiikabili Maabara hiyo ikiwemo vifaa na utaalamu wa kiufundi unaokubalika kufikia viwango vinavyotakiwa na Bodi ya Ithibati ya Kimataifa. 

Mohamed ameongeza kuwa kutunukiwa cheti hicho ni uthibitisho rasmi kuwa kuanzia sasa matokeo ya uchunguzi yanayotolewa na maabara ya Hospitali ya Mnazimmoja yanaweza kutumika na kuaminika nchi zote. 

Aidha amesema wananchi watajenga imani na huduma za uchunguzi wa maradhi mbali mbali zinazofanywa na maabara ya Mnazimmoja kwa vile imefikia kiwango cha Kimataifa. Faida nyengine itakayopatikana kutokana na cheti cha Ithibati ya Kimataifa amesema ni kutoa fursa kwa Taasisi za kimataifa na wasomi duniani kuitumia maabara hiyo kufanya tafiti mbali mbali zinazohusiana na Afya ya binadamu. 

Katika kuthamini cheti hicho, Dkt. Muhamed ameishauri Serikali kuziimarisha maabara za Hospitali nyengine kubwa na zile za Wilaya ikiwemo Makunduchi, Kivunge, Abdalla Mzee Mkoani, Chake chake, Wete na Vitongozi. 

Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya SADCAS Maureen Mutasa ameupongeza uongozi wa maabara ya Mnazimmoja kwa juhudi kubwa walizochukua licha ya kukabiliana na changamoto nyingi kabla ya kupata mafanikio hayo. Amesema cheti hicho ni cha 15 kutolewa na Bodi ya Ithibati ya SADCAS na kwa Tanzania ni maabara ya sita kupata cheti cha Ithibati maabara tano zipo Tanzania Bara. 

Hata hivyo ameushauri uongozi na wafanyakazi kwa jumla kuongeza juhudi za kutoa huduma bora ili cheti hicho ambacho kitadumu kwa miaka mitano kiendelee kubaki. 

Akipokea cheti cha Ithibati, Waziri Afya Mahmoud Thabit Kombo amewataka wananchi kuthamini juhudi zinavyofanywa na wafanyakazi wa vitengo mbali mbali vya Hospitali Kuu ya Mnazimmoja na kuacha tabia ya kulaumu. 

Ameushauri Uongozi na wafanyakazi wa Maabara hiyo kuendelea kuwahudumia wananchi kwa juhudi zao zote kwani juhudi hizo ndizo zilizopelekea kupewa cheti na kutambulika kimataifa.


Post a Comment