Thursday, September 15, 2016

HAKUNA MDORORO WA UCHUMI NCHINI – PROF. NDULU

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Prof. Benno Ndulu akitoa ufafanuzi kuhusu hali ya kukua kwa uchumi nchini kukanusha taarifa za kuwepo kwa mdororo wa uchumi nchini Tanzania.Kulia ni Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mabenki Bw. Kenedy Nyoni.

Na Lilian Lundo na Abushehe Nondo- MAELEZO.
Dar es Salaam.

14/9/2016. Dar es salaam.

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Prof. Benno Ndulu amesema kuwa hakuna mdororo wa uchumi nchini bali uchumi wa Tanzania umeendelea  kukua kwa kiwango cha asilimia 5.5 kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2016.

Aidha, amesema kuwa Tanzania ni kati ya nchi kumi bora za Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa kasi ya haraka.

Prof. Ndulu ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya hali ya uchumi nchini.

“Kwa mujibu wa Takwimu ya Ofisi ya Takwimu ya Taifa, hali ya ukuaji wa wa Tanzania imeendelea kuwa ya kuridhisha, ambapo katika robo ya kwanza ya mwaka 2016, ukuaji wa pato la Taifa unakadiriwa kuongezeka kwa asilimia 5.5” Prof. Ndulu.

Prof. Ndulu amezitaja shughuli zinazochangia kasi ya ukuaji wa uchumi kuwa ni pamoja na sekta ya, kilimo asilimia 11.7, biashara asilimia 10.6, uchukuzi asilimia 10.1, fedha asilimia 10.1 na mawasiliano asilimia 10.0.

Kwa mujibu wa Prof. Ndulu amesema shughuli za kiuchumi zilizokua kwa kasi ya juu zaidi katika robo ya kwanza ya mwaka 2016 ni sekta ya fedha asilimia 13.5, mawasiliano asilimia 13.4 na utawala wa umma asilimia 10.2.

Kuhusu mchango wa Sekta mbalimbali katika kuchangia kuleta fedha za kigeni nchini amesema kuwa Kilimo cha mazao yote kinachangia asilimia 25 ambazo ni dola za Kimarekani milioni 850, Utalii ukiongoza kwa dola bilioni 2.5, Viwanda dola bilioni 1.5 na dhahabu dola bilioni 2.5, usafirishaji kwenda nje bilioni 1.1.  
 
Akizungumzia  deni la Taifa, Prof. Ndulu amesema kuwa  kiwango cha deni hilo kwa sasa ni asilimia 20 ya pato la Taifa ambayo si mbaya ikilinganisha na ukomo wa asilimia 50 ya Pato la Taifa.

Prof. Ndulu amebainisha kuwa kulingana na tafsiri ya uchumi kuhusu deni hilo, Tanzania bado ina nafasi kubwa ya kuendelea kukopa bila kuhatarisha ustahimilivu wa deni hilo.

Katika hatua nyingine, Prof. Ndulu ametoa ufafanuzi  kuhusu mapato katika bandari ya Dar es Salaam kuwa yameongezeka licha ya kupungua kwa uingizwaji wa mizigo kupitia bandari hiyo.

Kuhusu mfumuko wa bei, Prof. Ndulu amesema bei za bidhaa mbalimbali zimeendelea kushuka na kufikia asilimia 4.9 kwa mwezi Agosti, ambapo  kushuka kwa kiwango hicho kulichangiwa na bei zisizojumuisha vyakula na nishati.

Prof. Ndulu pia amesema Serikali inaendelea na umaliziaji na uendelezaji wa miradi mikubwa  ya  miundombinu ikiwa ni pamoja na mradi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (standard gauge), ujenzi wa bomba la mafuta la Uganda na upanuzi wa bandari ya Tanga.

Aliitaja miradi mingine kuwa ni pamoja na ujenzi wa kanda  maalum ya uwekezaji, mradi wa kuzalisha megawati 240 za umeme wa Kinyerezi II ambapo miradi hiyo itachangia katika kuimarisha uchumi wa nchi.

No comments: