Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (mbele) akiongoza kikao kati yake na kampuni inayojishughulisha na usambazaji wa vifaa na teknolojia katika utafutaji wa mafuta na gesi ya Schlumberger. Pia kikao hicho kilihusisha watendaji kutoka Wizara hiyo pamoja na taasisi zake likiwemo Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC), Shirika la Madini la Taifa(STAMICO), Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo akifuatilia kwa makini maelezo yaliyokuwa yanatolewa na Meneja Masoko kutoka kampuni ya Schlumberger, Abdul Adeshina (hayupo pichani) katika kikao hicho.
Meneja Masoko kutoka kampuni ya Schlumberger, Abdul Adeshina akielezea shughuli zinazofanywa na kampuni hiyo ikiwa ni pamoja na kusambaza vifaa na teknolojia kwa ajili ya utafiti wa mafuta na gesi nchini.
………………………………………………………………………………………………………..
Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo ametaka makampuni yanayojishughulisha na shughuli za utafutaji na uchimbaji wa gesi na mafuta nchini kuongeza kasi ya utafiti kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili sekta ya gesi na mafuta iweze kukua na kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi.
Profesa Muhongo alitoa kauli hiyo alipokutana na kampuni inayojishughulisha na usambazaji wa vifaa na teknolojia katika utafutaji wa mafuta na gesi ya Schlumberger yenye makazi yake jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujadili utendaji kazi wa kampuni hiyo.
Kikao hicho kilichofanyika jijini Dar es Salaam kilihusisha watendaji kutoka Wizara hiyo pamoja na taasisi zake likiwemo Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC), Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).
Alisema Tanzania kwa sasa ina utajiri mkubwa wa rasilimali ya gesi ambayo itachochea katika ukuaji wa uchumi wa nchi kupitia umeme wa uhakika utakaotumika katika viwanda na kuongeza ajira kwa vijana wa kitanzania.
Aliendelea kusema kuwa ili sekta ya gesi na mafuta iweze kuwa na mchango katika ukuaji wa uchumi wa nchi, Tanzania inahitaji wawekezaji watakaowekeza kwa kasi kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Alisisitiza kuwa serikali ipo tayari kushirikiana na mwekezaji yeyote mwenye nia ya kuwekeza kwenye sekta ya gesi na mafuta kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
“ Kama serikali tumedhamiria kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi zenye utajiri unaotokana na rasilimali za gesi na mafuta, hivyo tunapenda kushirikiana na wawekezaji kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa kutumia teknolojia ya kisasa,” alisema Profesa Muhongo
Profesa Muhongo aliihakikishia kampuni ya Schlumberger kuwa serikali itafanya kazi kwa karibu nayo na kutoa ushirikiano wowote utakaohitajika ili sekta ya gesi na mafuta iweze kukua kwa kasi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi.
Awali akizungumza katika kikao hicho Meneja Masoko kutoka kampuni ya Schlumberger, Abdul Adeshina alisema kampuni yake imekuwa imekuwa ikitoa mafunzo kwa wafanyakazi wa kitanzania asilimia 80 wanaofanya kazi katika kampuni hiyo.
Aliongeza kuwa kampuni hiyo imekuwa ikishirikiana kwa karibu na Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) katika shughuli za utafiti wa mafuta na gesi nchini na kusisitiza kuwa kampuni hiyo ipo tayari kutumia teknolojia na vifaa vyake katika kuboresha shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi nchini.
Comments