GAVANA AZINDUA MWONGOZO WA KWANZA WA KITAIFA WA ELIMU NA ULINZI KWA MTUMIAJI WA HUDUMA ZA FEDHA” (N-FEF)

bot1
Meza kuu ikifuatilia kwa makini yanayojiri katika kikao cha uzinduzi wa Mwongozo wa kwanza wa kitaifa wa elimu na ulinzi kwa mtumiaji wa huduma za fedha” (N-FEF).
bot2
Baadhi ya wadau waliohudhuria uzinduzi huo.
bot3
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania akieleza jambo wakati wa uzinduzi Mwongozo wa kwanza wa kitaifa wa elimu na ulinzi kwa mtumiaji wa huduma za fedha” (N-FEF).
bot4
Bi. Susan Rutledge, Mtafiti na Mshauri wa masuala ya fedha, akieleza umuhimu wa elimu ya masuala ya fedha kuelekezwa kwa wananchi.
………………………………………………………………………………………………………………………………………..
Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwa kushirikiana na Mfuko wa Kuendeleza Huduma za Kifedha Tanzania (FSDT), imezindua Mwongozo wa taifa wenye lengo la kuongeza uelewa kuhusu elimu ya mambo ya fedha kwa wananchi.
Uelimishwaji wa wananchi kuhusu mambo ya fedha utatekelezwa kupitia “Mwongozo wa kwanza wa kitaifa wa elimu na ulinzi kwa mtumiaji wa huduma za fedha” (N-FEF).
Gavana Prof. Beno Ndulu ameuzindua rasmi mwongozo huu ambao utajikita katika kutatua changamoto zilizobainishwa katika utafiti uliopima uelewa wa mambo ya fedha kwa watu wazima nchini Tanzania. Utafiti huu unaitwa “Uwezo wa Kifedha Tanzania” wa mwaka 2014.
Utafiti huo umebainisha kuwa watanzania wengi hawana elimu na ujuzi mahususi wa  masuala ya mambo ya fedha kwa ujumla, hivyo kuwanyima fursa ya kutumia huduma za kifedha kwa faida yao.
Katika utafiti huo imeonyeshwa kuwa upatikanaji wa huduma za fedha umekuwa na changamoto katika maeneo mengi huku zile zitolewazo kwa njia ya mitandao bado hazikidhi matarajio ingawa zinawafikia  wateja wengi kwa sasa.
Sambamba na hilo kumekuwa na uhaba wa nyenzo na miundombinu ya kuhifadhi na kufikisha taarifa za fedha kwa watumiaji wa huduma hizo  kwa kuzingatia namna sahihi ya kutoa taarifa, kuwaelimisha na kuwalinda.
Kutokana na utafiti wa “Uwezo wa Kifedha Tanzania” wa mwaka 2014 wananchi kutoka makundi mbalimbali katika jamii hawana ujuzi wa hesabu za kawaida  ambao ndiyo msingi mkuu katika nadharia ya masuala yahusuyo mambo ya fedha. 
Elimu msingi katika masuala ya fedha umekuwa kikwazo kwa waliowengi  hasa katika uandaaji wa bajeti, kutunza kumbukumbu ya matumizi, kupanga fedha kwa matumizi yasiyotegemewa ama ya ziada na muhimu zaidi kutunza kiasi kwa ajili ya matumizi ya uzeeni (baada ya kustaafu).
Inaonekana kuwa upatikanaji wa taarifa za masuala ya fedha hutegemea zaidi vyombo vya habari kama redio, televisheni na magazeti lakini vyombo hivi kwa sehemu kubwa,  hufikisha zaidi taarifa za biashara na masoko kuliko ambavyo vinaelimisha jamii kuhusu matumizi na upangaji wa mapato yao.
 “Haya ndiyo masuala mahususi ambayo  mwongozo huu wa taifa kuhusu elimu ya huduma za fedha unalenga kushughulika nayo,” alisema Prof Ndulu.
Pamoja na kuwepo ongezeko la upatikanaji wa huduma za kifedha, mpaka asilimia 58  mwaka 2013 kutoka kiwango cha asilimia 17 mwaka 2009, miongoni mwa watu wazima nchini, bado mwongozo huu ni muhimu ili kuleta mfumo imara wa sekta ya fedha na Zaidi sana ili kuleta ustawi wa maisha ya watanzania kwa ujumla.
Prof. Ndulu anasema kutatua changamoto za kielimu kwa ujumla na hususan elimu ya huduma za fedha italiwezesha taifa kuwa katika mwelekeo mzuri wa kukabiliana na umasikini na kufikia malengo ya kukuza uchumi.
 “Tunapaswa kujiuliza: ni kwa namna gani wananchi hasa wale masikini na wasiokuwa na elimu za kifedha  za wanapambana kuendeleza biashara zao katika mazingira ya soko huria na lenye ushindani kila uchwao” alisisitiza Prof. Ndulu.
Hivyo, mwongozo huu utahakikisha watanzania wapata elimu sahihi na ya uhakika ya huduma za kifedha pamoja na njia anazoweza nazo kujilinda katika ushindani huu.
Vilevile mwongozo huu umeundwa ili kutatua changamoto za kifedha zinazohusiana na maamuzi miongoni mwa watumiaji wa huduma hizi na kuwa jumuishi na wenye tija kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Mwongozo wa taifa kuhusu elimu ya huduma za fedha umeandaliwa kwa kujumisha washikadau kutoka Tanzania bara na Zanzibar.
Unabainisha changamoto zinazohusuana na uwezo wa kifedha ambazo zinahitaji kutatuliwa kwa uwepo wa elimu ya fedha. Pia, unatoa taratibu wakufanikisha utekelezaji wa elimu ya fedha, na mwongozo wa kitaifa wa kuratibu elimu ya fedha nchini.
Lengo la mwongozo wa elimu ya huduma za fedha ni kuwa na wananchi na kaya zenye uwezo kifedha nchini.

Comments