Waziri wa nchi ofisi ya rais TAMISEMI, utumishi na utawala bora, George Simbachawene wa kwanza kushoto akiwaambia jambo mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo wa katikati na wa kulia mganga mkuu hospital ya Rufaa ya Tumbi dk. Peter Datan wakati alipotembelea shirika la elimu Kibaha juzi. (Picha na Mwamvua Mwinyi)
………………………………………
Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
Waziri wa nchi ofisi ya rais TAMISEMI, utumishi na utawala bora, George Simbachawene amesema ataunda tume ya watu wachache kutoka wizara hiyo haraka iwezekanavyo ili kuchunguza idara na vitengo vyote katika shirika la elimu Kibaha (KEC) ndani ya wiki mbili.
Amesema amefikia hatua hiyo baada ya kubaini tatizo kubwa la uongozi hivyo ipo haja ya kuchunguza hali iliyopo kuanzia juu hadi chini.
Aidha Simbachawene alisema tume hiyo itakuwa na kazi ya kupita kila idara na kitengo kuchunguza mambo atakayoyaelekeza kwa siku 14 kisha mwezi march mwaka huu atarejea kufanya ziara na kuzungumza na watumishi.
Alielezea kuwa kuna kila sababu ya kutafakari muundo mzima wa shirika na kuweka mikakati, sheria na mipango ya kisasa na kuondokana na ile iliyopitwa na wakati.
Aliyasema hayo juzi katika ziara yake ya kikazi ya siku moja aliyoifanya shirika la elimu Kibaha ambapo alipata fursa ya kutembelea maeneo ya uwekezaji na shirika kijumla.
Simbachawene alisema katika shirika hilo kuna wachache wanaonufaika na kuneemeka kwa kula hadi wamevimbilwa huku wengine wakiwa wanadidimizwa kimaslahi na kukosa haki zao za msingi
Comments