WAZIRI MKUU ATINGA BANDARI YA TANGA

tan1
Waziri  Mkuu Kassim Majliwa akizungumza na Mkuu wa bandari ya Tanga, Henry Arika (kulia kwake ) na  Mhandisi wa Mamlaka  ya Bandari Tanzania Felix Mahangwa ( kulia wakati alipotembelea bandari ya Tanga Februari 19, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
tan2
 Waziri Mkuu, Kssim Majaliwa akiongozwa na Mkuu wa Bandari ya Tanga , Henry Arika (kulia kwake) kukagua  bandari hiyo Februari 19, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
tan3
Matishari matatu ambayo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametaka apewe maelezo kwa  maandishi kuwa ni nani aliyeidhinisha mchakato wa manunuzi yake bila kuzingatia viwango na ubora uliokusudiwa na serikali. mheshimiwa Majaliwa alifanya ziara katika bandari ya Tanga Februari 19, 2016. (Picha na ofisi ya Waziri Mkuu)
………………………………………………………………………………………………………………….
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa leo jioni (Ijumaa, Februari 19, 2016) amekagua bandari ya Tanga na kumtaka Mkuu wa Bandari ya Tanga (Port Master), Bw. Henry Arika amletee maelezo juu ya ukiukwaji wa manunuzi ya tishari ifikapo kesho (Jumamosi) saa 6 mchana.
Waziri Mkuu ambaye aliwasili Tanga leo mchana ili kushiriki mazishi ya baba mzazi wa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bi. Ummy Mwalimu yaliyofanyika kwenye makaburi ya Mchukuuni, Tanga, aliamua kuzuru bandari hiyo kabla ya kuelekea uwanja wa ndege akiwa njia njiani kurejea Dar es Salaam.
Katika ziara hiyo fupi, Waziri Mkuu alikataa kuingia ofisini (bandarini) na akataka apelekwe mahali tishari tatu za bandari hiyo zilipo. Katika maswali aliyoulizwa na Waziri Mkuu, Bw. Arika alikiri kuwa matishari hayo hayafanyi kazi kama inavyotakiwa kwa sababu yanasubiri kusukumwa na tugboat  (meli ndogo).
“Nataka kesho saa 6 mchana uniletee barua yenye maelezo ni kwa nini mlinunua tishari tatu ndogo badala ya mbiili kubwa wakati mnajua Serikali ilitenga Dola za Marekani milioni 10.113 kwa ajili ya kununua tishari mbili zenye uwezo wa kujiendesha zenyewe  (self propelled) “
“Nataka maelezo ni kwa nini mlizinunua tangu mwaka 2011 lakini zimekaa bila kufanya kazi hadi Novemba mwaka jana? Na kwa nini mnaendelea kutumia hela ya Serikali kwa kukodisha tishari kutoka Mombasa badala ya kutengeneza za kwenu au kufundisha vijana wa Kitanzania? Kwani tunao wahitimu wangapi wa fani hii?” alihoji Waziri Mkuu
“Taarifa nilizonazo ni kwamba moja ya tishari lilidondoka baharini mkaenda kutafuta huko na kulivuta hadi hapa ndiyo maana yameshindwa kufanya kazi inavyotakiwa,” aliongeza.
Katika majibu yake, Bw. Arika alisema wao waliagiza tishari hizo kupitia ofisi ya Bandari makao makuu ambayo iko Dar es Salaam. “Pia wakati zinaagizwa sikuwepo hapa Tanga. Nimekuja mwishoni mwa mwaka jana,” alisema Mkuu huyo wa Bandari ambaye inaelezwa alitokea Mamlaka ya Bandari Dar es Salaam.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Bibi Mwantumu Mahiza awaite watu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Mamlaka ya Bandari na Jeshi la Polisi wakae na kutafuta mbinu za kudhibiti njia za panya zinazotumika kupitisha sukari ya magendo.
“Mkuu wa Mkoa simamia hawa watu, msaidiane kudhibiti uingizaji wa sukari kwa njia za panya. Kuna majahazi yanaleta sukari kutoka Brazil. Mheshimiwa Rais amepiga marufuku uingizaji wa sukari kutoka nje ili viwanda vyetu vya ndani viweze kuongeza uzalishaji. Dhibitini bandari zote ndogondogo hadi Pangani,” alisema Waziri Mkuu.
Alisema changamoto inayoikabili Serikali ni kwamba hata Shirika la Viwango Tanzania (TBS)  au Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) hawawezi kuzikagua sukari hizo na hazijulikani ubora wake licha ya kuwa zinafika kwa walaji.
Waziri Mkuu amerejea jijini leo jioni.

Comments