RAIS MHE.DKT. MAGUFULI AFANYA MAZUNGUMZO NA KATIBU MTENDAJI WA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI DKT. RICHARD SEZIBERA


 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akimkaribisha Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Dkt. Richard Sezibera Ikulu jijini Dar es Salaam.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Dkt. Richard Sezibera Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Dkt. Richard Sezibera mara baada ya kumaliza mazungumzo Ikulu jijini Dar es Salaam .PICHA NA IKULU





JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU



Simu: 255-22-2114512, 2116898
E-mail: press@ikulu.go.tz
Tovuti : www.ikulu.go.tz              

Faksi: 255-22-2113425






Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Dkt. Richard Sezibera Ikulu Jijini Dar es salaam, ambapo pamoja na mambo mengine Rais Magufuli amepokea taarifa ya maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki utakaofanyika tarehe 02 Machi, 2016 Katika Jiji la Arusha, Nchini Tanzania.

Rais Magufuli ndiye Mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki inayojumuisha nchi tano wanachama ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.Akizungumza mara baada ya mazungumzo hayo Katibu Mtendaji wa Jumuiya hiyo Dkt. Richard Sezibera, amesema maandalizi kuhusiana na mkutano huo yanakwenda vizuri.

Amesema pamoja na mambo mengine mkutano huo, utajadili masuala kadhaa yakiwemo mpango wa kuanzisha viwanda vya magari ndani ya Jumuiya ili kupunguza uingizaji wa magari kutoka nje ya nchi na Marais kuzindua pasi ya kusafiria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.Kuhusu hali ya Jumuiya, Dkt. Sezibera amesema inaendelea vizuri na ametaja baadhi ya mambo ambayo yamefanyika kuwa ni kutiwa saini kwa mkataba wa umoja wa forodha, makubaliano ya soko la pamoja na makubaliano ya sarafu moja.
Mengine ni kuwepo kwa mazungumzo kuhusu uimarishaji wa miundombinu kama vile reli na umeme ndani ya Jumuiya, na  mazungumzo kuhusu umoja wa kisiasa.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Dkt. Augustine Mahiga, amesema Tanzania ikiwa ni mwenyeji wa kikao hicho ipo tayari kupokea ugeni na kwamba pamoja na kufanyika kwa kikao hicho, marais wa Tanzania na Kenya watafungua barabara inayounganisha Tanzania na Kenya katika Mpaka wa Holili na kutakuwa na shughuli ya kuweka jiwe la msingi katika kituo cha pamoja cha mpakani kwa ajili ya kuwezesha upitaji wa mizigo na watu yaani "One Stop Boarder Post"

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU.
Dar es salaam
24 Februari, 2016

Comments