Mwenyekiti wa UDP Mh. John Cheyo akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani)kwenye ukumbi wa Idara ya Habari MAELEZO mapema leo jijini Dar,akiwaomba viongozi wa chama cha CHADEMA,Kusitisha maandamano yao waliyoyapa jina la UKUTA,wanayotarajia kuyafanya Septemba Mosi nchi nzima,Mh Cheyo amekiomba chama hicho kutofanya maandamano hayo kwa lazima na badala yake watumie njia ilio sahihi ambayo ni ya mazungumzo ya mezani na kuendelea kuitunza amani ya nchi iliopo,pia amewaomba Watanzania kupaza sauti zao kuyakataa maandamano hayo yanayoweza kuharibu amani na utulivu wa nchi yetu.Pichani kulia ni Kaimu Katibu MKuu wa chama hicho Mh,Goodluck Ole Medeye.
"Ukitaka kufanya maandamano,vyombo vya usalama vikikukatalia,basi usitumie nguvu,jaribu kutafauta njia nyingine ambayo itakuwa ya amani zaidi kuliko kulazimisha,jambo ukililazimisha bila kufuata taratibu na sheria za nchi,matokeo yake hayatakuwa mazuri,yataleta machafuko na kutia doa amani ya nchi yetu ambayo tumekuwa tukijivunia,hivyo nawasihii ndugu zangu wa CHADEMA bado kuna njia nzuri za kufuata na kufikia muafaka wa jambo hilo bila kusumbua amani ya nchi yetu iliopo kwa sasa" alisema Mh Cheyo.
Mh,Cheyo akisitiza jambo wakati alipokuwa akijiabu maswali mbalimbali ya waandishi wa habari waliohudhuria mkutano huo wa kukitaka chama cha CHADEMA kusitisha maandamano yake,kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari MAELEZO,Vicent Tinganya.PICHA NA MICHUZI JR.
Na: Lilian Lundo-MAELEZO
Dar Es Salaam
Mwenyekiti wa Chama cha UDP John Cheyo amewataka Watanzania kupaza sauti na kukataa maandamano ya Septemba Mosi mwaka huu ambayo yameandaliwa na Chama cha Demokrasia (CHADEMA).
Cheyo ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu msimamo wake juu ya maandamano hayo.
“Watanzania wenzangu jambo la kuwaacha watoto wetu kwenda kupambana na Polisi si jambo zuri, wote tupaze sauti zetu na kusema hapana kwa maandamano ya Septemba Mosi,” alisisitiza Cheyo.
Alisema kuwa, ziko njia mbalimbali ambazo Chadema wanaweza kuzitumia kutatua migogoro, kama vile meza ya mazungumzo na kuachana na maandamano ambayo yanachochea vurugu na hata kutishia amani ya nchi.
Aliongeza kuwa Jeshi la Polisi linapotoa katazo la maandamano ni lazima utii uwepo, kwani Polisi wapo kwa mujibu wa Sheria na Katiba. Ikiwa Chama hicho hakikuridhika na katazo hilo basi wanatakiwa kuonana na Waziri anayehusika na Jeshi la Polisi.
Akifafanua zaidi alisema kuwa Rais Magufuli amekuwa akichukua hatua za makusudi za kutatua matatizo mbalimbali kama vile kupambana na ufisadi, ambapo viongozi wengi wa Serikali wamesimamishwa kazi au kufukuzwa kutokana na kujihusisha na masuala ya rushwa.
Mwenyekiti huyo wa UDP amewataka watanzania kumuunga mkono Mhe. Rais Magufuli ili aweze kutimiza ndoto zake na yale ambayo ameyaahidi kwa ajili ya nchi ya Tanzania.
Aidha Cheyo aliwasifu viongozi wa Dini ambao walikaa na Viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) na kukubali kurudi bungeni bila pingamizi lolote. Amewataka viongozi hao wa dini kuendelea kuzungumzia suala la amani kwa Watanzania na Viongozi wa kiasa ili kudumisha amani ya nchi.
Comments