Thursday, August 04, 2016

MOI yatoa sababu ya kuongezeka kwa msongamano wa wagonjwa

1 (5) Idadi ya wagonjwa wa upasuaji katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) imeongezeka kutoka wagonjwa 20 mpaka wagonjwa 40 kwa siku.
Meneja Ustawi wa Jamii na Uhusiano wa taasisi hiyo Jumaa Almas ameyasema hayo leo, jijini Dar es Salaam wakati akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari juu ya tuhuma zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa taasisi hiyo inabana matumizi na kusababisha msongamano wa wagonjwa taasisi hiyo.
Amesema asilimia 80% ya wagonjwa walio katika taasisi hiyo wanahitaji upasuaji wa dharura jambo ambalo limeilazimu taasisi hiyo kufungua wodi nyingine ya upasuaji ili wagonjwa wote wanaohitaji huduma ya upasuaji wa dharura waweze kufanyiwa ili kuokoa maisha yao.
“Msongamano wa wagonjwa MOI hausababishwi na kubana matumizi bali ni kutokana na kuongezeka kwa wagonjwa kutoka wagonjwa 20 mpaka wagonjwa 40 kwa siku ambapo kumesababishwa na ongezeko kubwa la ajali hasa za pikipiki katika jiji la Dar es Salaam,” amesema Almas.
Amefafanua kuwa wagonjwa wa upasuaji wa kichwa na ubongo hulazimika kusubiri kwa muda kutokana pindi wanapopelekwa katika chumba cha wagonjwa mahututi mara baada ya upusuaji na kuongeza kuwa vyumba vya wagonjwa mahututi ni vichache ikilinganishwa na ongezeko kubwa la wagonjwa wanaohitaji upasuaji huduma hiyo.
Amesema taasisi hiyo inategemea kuongeza vyumba vingine zaidi kwa ajili ya wagonjwa mahututi ili kukidhi idadi ya wagonjwa ambao wamekuwa wakiongezeka kila siku
Akifafanua kuhusu usitishwaji wa kambi za upasuaji (surgical camps) zilizokuwa zikifanyika siku za mapumziko amesema kuwa kambi hizo zimesitishwa kwa muda mrefu kufuatia uamuzi wa Bodi ya wadhamini ya MOI baada ya bajeti ya kuendesha kambi hizo kuwa kubwa ikilinganisha na mapato ambayo taasisi imekuwa ikiyapata ambayo yamekuwa yakiigharimu Taasisi hiyo kiasi cha shilingi milioni 5 mpaka 7 kwa wiki.
Pia amekanusha suala la uuzwaji wa viungo pandikizi katika Taasisi hiyo na kusisitiza kuwa sio la kweli bali Taasisi imekuwa ikipata msaada wa vipandikizi hivyo kutoka Taasisi ya Sign Group International ya Marekani kwa miaka mitano sasa na wagonjwa wamekuwa wakichangia gharama za upasuaji, dawa na huduma nyingine.
Amesisitiza kuwa Uongozi MOI unawahakikishia watanzania kwamba huduma taasisi hiyo zinaendelea kama kawaida na yoyoye mwenye malalamiko juu ya huduma ya MOI afike ofisi ya Uhusiano na Ustawi wa Jamii na malalamiko yake yatashughulikiwa.

No comments: