VYUO VIKUU VILIVYOPOKEA FEDHA AMBAZO WANAFUNZI HAWAPO CHUONI VYAPEWA SIKU SABA KUREJESHA FEDHA HIZO


Na: Lilian Lundo na Sheila Simba - MAELEZO



Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof.  Joyce Ndalichako ametoa siku saba kuanzia Agosti 17, 2016 kwa vyuo vikuu kurejesha fedha zilizopokea ambazo ni za wanafunzi ambao hawapo chuoni.



Prof.  Ndalichako ameyasema hayo leo, jijini Dar es Salaam alipokuwa akiongea na waandishi wa habari juu ya taarifa la zoezi la uhakiki wa wanafunzi wanufaika wa mikopo vyuo vya Elimu juu.



Prof.  Ndalichako amesema kuwa uhakiki wa wanafunzi hao umefanyika katika vyuo 31 kati ya vyuo 81 vilivyopo nchini, Katika utafiti huo wanafunzi 2,192 wameshindwa kuhakiki majina yao, hivyo kushindwa kuthibitisha uwepo na uhalali wa wanafunzi hao.



“Mikopo ya Wanafunzi hao imesitishwa na kwa wale ambao ni wanafunzi halali lakini walishindwa kujihakiki itabidi waombe tena mkopo,” alifafanua Mhe. Ndalichako.



Ameendelea kwa kusema kuwa, kwa mwaka wa fedha 2015/16 wanafunzi hao hewa wameigharimu Serikali kiasi cha shilingi 3,857,754,460, kiasi ambacho kinatakiwa kurejeshwa na vyuo ambavyo wanafunzi hao wamebainika.



Aidha, Prof.  Ndalichako amesema kuwa taarifa hiyo imekabidhiwa kwenye vyombo vya sheria ili kuwachukulia hatua wale wote watakaobainika kufanya  udanganyifu na kusababisha Serikali hasara ya mabilioni ya fedha.



Vile vile Prof. Ndalichako amewataka wakuu wa vyuo kuweka mfumo wa kuhakiki usahihi wa matokeo ya wanafunzi yanayotumwa Bodi ya Mikopo  kutokana na vyuo vingi kubainika kuwepo kwa udanganyifu mkubwa kwenye matokeo ya wanafunzi ambao hawakufanya mtihani au waliofeli na kuandikiwa wamefaulu ili waendelee kupata mikopo.

Comments