TAMASHA la wasanii wa kizazi kipya la kuchangia madawati limefanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa Dar Live Mbagala ambapo jumla ya madawati 150 yamepatika.
Tamasha hilo liliandaliwa na Mkuu wa Wilaya ya Handeni Godwin Gondwe ‘Double G’ ambapo aliwashukuru wasanii hao kwa kujitokeza kusapoti upatikanaji wa madawati kwa watoto wa Handeni ambao ni moja ya changamoto zinazokabili Wilaya yake ukiachilia ile ya Maji.
Wasanii waliojitokeza kuunga mkono juhudi za Mkuu huyo wa Wilaya ya Handeni walisema wameamua kumsapoti Gondwe kwa kuwa wanamfahamu muda mrefu toka akiwa mtangazaji wa radio na alikuwa akiwasapoti kazi zao kwa kiasi kikubwa.
Ben Paul alisema “Wasanii kama wasanii tunatakiwa tusaidie jamii yetu kama hivi, naishi kwenye jamii hivyo naona matatizo mengi yanayokabili jamii yetu ni wajibu wangu kutumia nafasi hii kusaiii, karne hii wadogo zetu bado wanakaa chini, tunatakiwa kushirikiana kwa pamoja kumaliza tatizo hilo.”alisema Ben Paul anayetamba na Wimbo wake wa sasa wa ‘Moyo Mashine’ na kuongeza.
“Vijana wa sasa wanapenda kushinda kwenye mitandao ya kijamii na kulalamikia serikali, wanataka serikali ndio iwafanyie kila kitu wakati sisi hatufanyii jambo serikali.”alisema.
Msanii nguli, Ambwene Yesaya ‘Ay’ akizungumzia tamasha hilo alisema “Double G kwanza kabisa ni mtu wa watu, ndio maana wasanii wote unaotuona hapa tumeamua kumsapoti bure kabisa, alivyotueleza wazo lake tukamwambia ni zuri na tutamsapoti, alichokifanya ni kitu kizuri ambacho kinatakiwa kiigwe na kila mtu.
“Itakuwa vizuri kila mtu akaweka nia ya kusaidia sio lazima tutengeneze madawati tunaweza tukafanya siku ya kuotesha miti ambayo naamini kila msanii akiotesha mti mmoja leo, utakuwa na manufaa kwa vizazi vijavyo.”alisema Ay.
Aidha mwandaaji wa tamasha hilo Godwin Gondwe alisema kuwa Wilaya yake inakabiliwa na uhaba wa madawati 530 na anashukuru kwa kupata madawati 150 katika fedha zilizopatikana kwenye tamasha hilo la Wasanii hna kwamba bado ana upungufu wa madawati 380.
“Nawashukru sana wasanii waliojitoa kunisapoti, na wakazi wa Wilaya ya Temeke kujitokeza kumuunga mkono Rais wetu ili kutengeneza historia za wadogo zao wasikae chini tena, na katika tamasha hili tumeweza kukusanya fedha ambazo zitatuwezesha kupata madawati 150.”alisema Gondwe.
Katika tamasha hilo, muitikio wa watu ulikuwa mkubwa na lilipendezeshwa na wasanii mbalimbali. Walioanza kufanya makamuzi mwanzoni mwa tamasha hilo ni pamoja na Bendi ya La Musica Vijana Classic, Mc wa Dar Live Brighton ‘Dalada’ na wengine wengi.
Baada ya shoo kunoga mashabiki wa Dar Live walifurahia muziki mzuri kutoka kwa Bendi ya Injili ya GWT (Glorious Worship Team), Mfalme wa Muziki wa Uswazi maarufu kama Singeli Msaga Sumu, Sterio, Ben Pol, Linex huku Fid Q, AY, Msami na Barnaba wakikamilisha listi kwa makamuzi ya nguvu.
Baada ya wasanii wote kutoa burudani ya nguvu, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe ‘Double G’ aliwashukuru wote waliomuunga mkono na akaomba waendelee kujitolea zaidi kwenye masuala ya kujenga taifa.
Comments