*Shinzo Abe aahidi $ bilioni 10 kwa miaka mitatu
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema mabadiliko ya mifumo ya ujenzi wa uchumi wa viwanda hayawezi kuletwa na Serikali peke yake bali ni lazima yahusishe pia wadau kutoka sekta binafsi.
“Tunahitaji kushirikiana na sekta binafsi ili tuweze kufanikisha ajenda zetu za maendeleo ziwe za kitaifa, kikanda au za bara zima la Afrika. Ushirikiano huu utasaidia kuleta mabadiliko dhahiri ya kiuchumi na kukuza ustawi wa jamii zetu,” alisema.
Ametoa kauli hiyo jana (Jumamosi, Agosti 27, 2016) wakati akichangia mjadala kuhusu TICAD na umuhimu wake kwa maendeleo ya Afrika mara baada ya ufunguzi wa Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Bara la Afrika (TICAD VI) uliofanyika katika kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Jomo Kenyatta (JICC) jijini Nairobi, Kenya.
“Wakati Serikali zinaweka mazingira wezeshi ya kufanya biashara na uwekezaji, jukumu kubwa la sekta binafsi ni kuleta mageuzi ya kiuchumi na kujenga uchumi wa viwanda ambao ndio tunakusudia kuufikia,” alisema.
Waziri Mkuu ambaye anahudhuria mkutano huo wa siku mbili kwa niaba ya Rais, Dk. John Pombe Magufuli, alisema Tanzania inawakaribisha wawekezaji wa sekta binafsi kutoka Japan waje kujenga viwanda vya kusindika gesi asilia, kutengeneza mbolea na kemikali mbalimbali, vyuma, nguo, bidhaa za ngozi na usindikaji wa mazao.
Alisema ili kufikia uchumi wa viwanda na maendeleo endelevu, ni lazima nchi za Afrika na wabia wa TICAD wawekeze kwa pamoja na washirikiane kujenga uwezo wa rasilimali watu, kwa kuwa ndio nguzo muhimu ya kuleta ushindani wenye tija katika sekta ya viwanda.
Akizungumzia mpango wa mafunzo kwa vijana wa Kiafrika katika masuala ya biashara (African Business Education Initiative for Youth–ABE), Waziri Mkuu alisema: “Huwezi kuzungumzia mabadiliko ya mfumo wa uchumi wa viwanda bila kujenga uwezo wa watu wetu ambao hasa ndiyo watekelezaji wa mabadiliko hayo. Ni lazima pia tuangalie vipaumbele vya kidemografia kama kweli tunataka kukuza uchumi kwa kujenga tabaka la watu wenye ujuzi.”
Mapema, Waziri Mkuu wa Japan, Bw. Shinzo Abe aliwaahidi viongozi wa nchi za Afrika kwamba nchi yake itatoa kiasi cha dola za marekani bilioni 10 katika kipindi cha miaka mitatu kwa ajili ya kuendeleza miundombinu barani humo na kwamba sehemu ya fedha hizo itatolewa kwa kushirikiana na Benki ya Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB).
“Ahadi hii ina nia ya kuendeleza miundombinu ya barabara, bandari na nishati jadidifu hasa ya nishati ya jotoardhi kwani bara hili lina uwezo mkubwa wa kuzalisha nishati hiyo kwa wingi,” alisema.
“Uzalishaji wa umeme barani Afrika, unatarajiwa kuongezeka kwa kiwango cha megawati 2,000. Nishati ya jotoardhi itaboreshwa kwa kutumia yeknolojia za Kiajapan. Na kutokana na mradi huo, utazalishwa umeme wa kutosha kuhudumia nyumba zaidi ya milioni tatu ifikapo mwaka 2022,” alisema.
Hii ni mara ya kwanza kwa mkutano wa TICAD kufanyika barani Afrika tangu mikutano hii ianze mwaka 1993. Mkutano huo, unahudhuriwa na washiriki zaidi ya 6,000 kutoka bara la Afrika na Japan.
Mkutano huo uliofunguliwa kwa pamoja na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe, umehudhuriwa na marais 34 kutoka nchi za Afrika, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Ban Ki-Moon na Marais wa Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB).
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, AGOSTI 28, 2016.
Comments