Friday, August 19, 2016

Madaktari Bingwa waendelea kuwahudumia wananchi Singida

Baadhi ya wakazi wa Iramba waliojitokeza siku ya siku ya kwanza ya huduma tembezi za kibingwa.
. Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew J. Mtigumwe akihutubiwa wakati wa uzinduzi rasmi wa huduma tembezi za madaktari bingwa Mkoani Singida.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida John Mwombeki akisoma taarifa ya hali ya afya Mkoa wa Singida wakati wa uzinduzi wa huduma tembezi za kibingwa
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Macho akimhudumia mteja siku ya kwanza ya huduma tembezi za kibingwa.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Meno akimhudumia mteja siku ya kwanza ya huduma tembezi za kibingwa.
 
Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew J. Mtigumwe amezindua rasmi huduma tembezi za madaktari bingwa Mkoani Singida, na kuwasihi wananchi Mkoani Singida kujitokeza kwa wingi kupata huduma hizo za kibingwa. 

Huduma hizo za kibingwa zilizozinduliwa Wilayani Iramba katika hospitali ya Kiomboi zitahusisha huduma za kibingwa za upasuaji, meno, macho, upasuaji wa mifupa, huduma za kibingwa za magonjwa ya watoto, wanawake na huduma za kibingwa za mionzi. 

Mhandisi Mtigumwe amesema matarajio ya Mkoa ni kuwa huduma tembezi za kibingwa zitasaidia kutambua na kutibu magonjwa mbalimbali kabla hayajafikia hatua ya usugu na kupunguza gharama za rufaa za wagonjwa kwenda nje ya mkoa. 

'Huduma tembezi za kibingwa zitawasaidia wananchi kutambua uwepo wa huduma za kibingwa katika mkoa wa singida na kupata matibabu kwa gharama nafuu' amengeza Mhandisi Mtigumwe. 

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa Dokta John Mwombeki akisoma taarifa ya hali ya afya Mkoa wa Singida amesema wazo la kuanzisha huduma tembezi za kibingwa limetokana na idadi kubwa ya operesheni zilizofanyika kwa mwaka 2015/2016 na pia mkutano wa wadau wa afya mkoani hapa kuafiki wazo la kuanzisha huduma hiyo. 

"Kwa kipindi cha mwaka 2015/2016 jumla ya operesheni kubwa na ndogo 4,836 zimefanyika katika hospitali mbalimbali mkoani hapa, aidha Idara ya macho katika hospitali ya Mkoa imefanya jumla ya operesheni kubwa na ndogo 2,020" ameongeza Dokta Mwombeki. 

Dokta Mwombeki amesema uwepo wa madaktari bingwa 11 mkoani Singida pia umekuwa chachu ya utekelezaji wa huduma hiyo huku Mkoa ukifanya jitihada za kuazima madaktari wengine katika mikoa jirani ya Dodoma na Manyara. 

Baadhi ya wagonjwa waliohudhuria katika siku ya kwanza ya zoezi hilo huku huduma hiyo ikitarajiwa kufanyika kwa muda wa siku tano wilayani hapo wameeleza shauku na furaha yao ya kusogezewa huduma za kibingwa katika halmashauri zao. 

"Nilikuwa naumwa jino ambalo limeota vibaya, niliambiwa nitaweza kufanyiwa operesheni katika hospitali kubwa kama Muhimbili lakini hawa madaktari wametusaidia , nimepata huduma haraka na kwa gharama nafuu, nawasihi wenzangu waje kwa wingi" amesema Bi Neema Josseph Mkazi wa Kijiji cha Kizaga Wilayani Iramba. 

Naye Mzazi wa mtoto Jonas Masaka amesema huduma za kibingwa zitamsaidia mtoto wake mwenye matatizo ya macho na hiyo kumpunguzia gharama ya kumpeleke katika hospitali kubwa kutibu tatizo la macho linalomsababisha mtoto huyo kushindwa kusoma vizuri. 

Huduma ya tembezi za kibingwa Mkoani Singida zitafanyika katika Wilaya zote tano za Mkoa nwa Singida na hvyo kupunguza wagonjwa wa rufaa watakaopelekwa hospitali za Bugando, KCMC na Muhimbili.
 
Post a Comment