NSSF YAMUUNGA MKONO RAIS DK. JOHN POMBE MAGUFULI KWA MKOPO WA SH.BILIONI NNE KWA KIWANDA CHA VIUADUDU KIBAHA

 Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya jamii (NSSF)Prof Godius Kahyarara (kulia) akikabidhi mfano wa hundi ya pesa yenye thamani ya dola za kimarekani milioni 2 na laki 1 (zaidi ya Tsh bilioni nne) kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC)  Dkt Samuel Nyantahe (wa tatu kushoto) ikiwa ni mkopo kwa ajili ya kuongeza uzalishaji kwenye kiwanda  cha kuzalisha  viuadudu vya kuua viluwiluwi vya mbu cha Tanzania Biotech Product  Ltd kilichopo wilayani Kibaha, mkoani Pwani wakati wa hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika mwishoni mwa wiki. Wanaoshuhudia ni pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (katikati), Mkuu wa wilaya ya Kibaha, Bi Assumpta Mshana, (wa pili kulia) Mkurugenzi wa huduma za sheria wa Benki ya Azania, Bw Geofrey Dimoso (wa pili kushoto) na Kaimu Meneja Mkuu wa kiwanda hicho Bw Samwel Mziray.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama Mkuu wa wilaya ya Kibaha, Bi Assumpta Mshana pamoja na  jopo la maofisa  kutoka NSSF, NDC, benki ya Azania na uongozi wa kiwanda cha kuzalisha  viuadudu vya kuua viluwiluwi vya mbu cha Tanzania Biotech Product kwa pamoja wakimsiliza mmoja wa wataalam kutoka kiwanda hicho aliekuwa akifafanua moja ya shughuli za kiwanda hicho.
  Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (kulia) akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya jamii (NSSF)Prof Godius Kahyarara (kushoto) pamoja na viongozi wa NSSF kwenye ziara hiyo.

Na Chalila Kibuda, Globu ya jamii.
SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limetoa mkopo wa dola za Kimarekani  mil. 2.1 (zaidi ya sh bilioni nne) kwa kiwanda  cha kuzalisha  viuadudu vya kuua viluwiluwi vya mbu cha Tanzania Biotech Product  Ltd kilichopo wilayani Kibaha, mkoani Pwani ili kukiongezea uzalishaji wake, hatua inayotajwa kuwa ni kuitikia wito wa Rais Dr John Magufuli wa kuifanyaTanzania kuwa nchi ya viwanda.

Mbali na mkopo huo unaotolewa kupitia benki ya Azania itayayosimamia urejeshwaji wake, pia shirika hilo lipo kwenye mchakato wa kuwekeza kwenye ujenzi wa viwanda vipya na vikubwa zaidi vya kutengezeza nguo, matairi pamoja na sukari hapa nchini.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu), Jenista Mhagama mbali na kulipongeza shirika hilo kwa kuunga mkono nia ya Rais na serikali kwa ujumla katika kuelekea uchumi wa viwanda, alisema uwezeshaji wa kiwanda hicho  umeongeza kasi ya vita dhidi ya ugonjwa wa Malaria kwa asilimia tisini (90).

“Kiwanda kipekee barani Afrika na ufanisi wake utawanufaisha si tu watanzania bali Waafrika kwa ujumla na kutuletea fedha za kigeni,  na kuweza kufikia uchumi wa kati katika sekta ya viwanda’’ alisema.

Amesema uamuzi wa shirika hilo kutoa mkopo huo kupitia benki ya Azania utaliwezesha shirika hilo kuwa na msimamizi thabiti wa marejesho ya pesa za wanachama wa mfuko huo.

“Mwanzo kabisa kwenye uamuzi huu  niliomba kupata uhakika fedha za wanachama na nilipohakikishiwa kuwa kuna benki itasimamia mkopo huu basi nikajua pesa za wanachama zipo salama. Niendelee tena kuwaomba wahusika wote wawe makini kwenye pesa hizi,’’ alisisitiza.

Alitoa wito kwa mifuko ya hifadhi hapa nchini kuhakikisha inawekeza zaidi kwenye viwanda huku akiwataka viongozi wa mashirika mbalimbali kuhakikisha wanalinda haki na maslahi ya wafanyakazi wao likiwemo suala la kuwaunganisha wafanyakazi wao na  mifuko ya hifadhi ya jamii.

Akizungumza wilayani Kibaha  wakati wa hafla fupi ya kukabidhi mkopo huo kwa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) linalomiliki kiwanda hicho, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Prof Godius Kahyarara alisema shirika lake lina dhamira ya dhati katika kuwekeza kwenye viwanda nchini ili kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi wa Tanzania.

“Pamoja na kuitikia wito wa Rais Dk.John Magufuli katika kuibadilisha Tanzania kuwa nchi ya viwanda ili kuiongeza ajira hapa nchini lakini pia tunatarajia kupata faida kupitia marejesho ya pesa hizi,’’ Alibainisha.

Akiwatoa hofu wanachama wa mfuko huo na watanzania kwa ujumla kuhusu usalama wa pesa zao, Prof Kahyarara alisema uamuzi wa shirika kuwekeza kwenye viwanda sio mgeni kwa kuwa ulianza miaka ya nyuma ambapo shirika hilo liliwezesha viwanda vya saruji Mbeya, Mkonge Tanga, Sukari Kagera na kiwanda cha nguo 21st Century cha Morogoro.

“Uwekezaji huo ulionyesha mafanikio makubwa kwa wananchi wengi walipata ajira na shirika lilipata faida iliyokusudiwa na kuboresha mafao ya wananchama.  Tupo makini na aina za uwekezaji na miongoni mwa kanuni tunazotumia katika uwezaji ni suala la tija, faida, usalama na malengo ya mradi husika hususani katika kuinua uchumi wa nchi kwa ujumla,’’ alisema.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya NDC Dkt Samuel Nyantahe alisema mkopo huo utakiwezesha kiwanda hicho ambacho kimejengwa kwa kushirikiana na kampuni ya LABIOFAM SA ya nchini Cuba kupanua uzalishaji wake na kuwa katika nafasi ya kutafuta soko hadi nje ya nchi.

Naye Mkurugenzi wa huduma za sheria wa Benki ya Azania, Bw Geofrey Dimoso alisema benki yake imejipanga kuhakikisha inasimamia urejeshwaji wa pesa hizo kwa mfuko wa NSSF huku akiwatoa hofu wanachama wa mfuko huo kuwa pesa zao zipo salama.

Comments